Mkulima
wa Shahiri pamoja na maofisa kilimo wa TBL wakikagua mashamba
Wabunge
wa Kamati ya BIashara na Kilimo walipotembelea mashamba ya wakulima wa zao la
Shahiri hivi karibuni.
Mkulima wa Shahiri Peter Nade akiwa amesimama kwenye trekta lake ni
mmoja wa wakulima waliofanikiwa chini ya mpango huu
**************
UTEKELEZAJI wa mpango wa
kufanya kazi kwa kushirikiana na wakulima wadogo wadogo ujulikanao kama Go Farming
ambao umeanza kutekelezwa na kampuni ya TBL Group kwa wakulima wa zao la
Shahiri kanda ya Kaskazini mwa Tanzania umesaidia kuongeza ajira ikiwemo
kuboresha maisha ya wakulima.
Afisa Mwandamizi wa TBL Group
anayesimamia mpango huo Bw.Optat Morrice amesema jana mjini Arusha kuwa
mpango wa Go Farming awamu ya kwanza unatekelezwa katika mikoa ya Arusha
na Kilimanjaro mbali na wakulima unanufaisha watanzania zaidi ya 3,000
wanaojipatia ajira katika utekelezaji wake.
Aliyataja makundi ya
wawaonufaika na mpango huu kuwa ni vibarua wanaofanya kazi mashambani kwa
kupuliza dawa mashambani,madereva wa matrekta wanaolima mashamba na
kuvuna,vibarua wa kupakia mazao na kuyashusha,wasafirishaji na watengenezaji na
magunia ya kupakia mazao.
Alisema Mbali na wanaonufaika
katika hatua mbalimbali za utekelezaji wakulima wa zao la Shahiri katika
mikoa ya Kaskazini ya Arusha na Kilimanjaro tayari wameanza kuonja
matunda ya ushirikiano huu kwa kuwa wanawezeshwa kuendesha kilimo cha
kisasa,kupatiwa pembejeo,mbegu na wataalamu wa kutoa ushauri na wanakuwa na
soko la uhakika kwa ajili ya kuuza mazao yao,hali ambayo imebadilisha hali zao
za maisha kuwa bora.
Morrice alisema lengo kubwa la
mpango huu ni kuinua maisha ya wakulima wadogowadogo,kuongeza kasi ya kukua
uchumi na kujenga mfumo mzuri na endelevu wa kupata malighafi kwa ajili
ya viwanda kampuni mama ya TBL Group ya SABMiller vilivyopo kwenye nchi
mbalimbali barani Afrika.
“Mpango wa Go Farming haulengi
kunufaisha wakulima wa Shahiri pekee bali pia wa mazao mengine kama mtama na
mihogo na katika siku za usoni wakulima wa zao la mahindi watawezeshwa pia na
inategemewa hadi kufikia mwaka 2020 zaidi ya wakulima nusu milioni watakuwa
wamewezeshwa sehemu mbalimbali duniani ambako kampuni imewekeza na mamilioni ya
wananchi watajipatia riziki kutokana na kufanya kazi za utekelezaji
wake”.Alisema Morrice.
Aliongeza kuwa matarajio ya
mafanikio ya mpango huu katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020 yanaonyesha
kukua kwa asilimia 44 katika nchi 10 ambako umeanza kutekelezwa na inakadiriwa
kuwepo ongezeko la uzalishaji wa mazao kutoka tani 300,000 kufikia zaidi ya
tani 600,000.
Mpango huu wa kampuni
kutegemea kupata malighafi kutoka hapa nchini umeungwa mkono na serikali
za nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania kwa kuwa unalenga kuinua hali za maisha za
wananchi hasa wakulima ambao wana hali duni,hali hii imepelekea baadhi ya nchi
kuipunguzia kodi ya zuio kampuni inapofanya uzalishaji kwa malighafi
zilizonunuliwa ndani ya nchi .
Hivi karibuni Kamati ya Bunge
ya Viwanda,Biashara ya Mazingira ilipata fursa ya kutembelea wakulima wa zao la
Shahiri wanaoshirkiana na TBL Group na baadhi ya wajumbe wa kamati hii
walipongeza mpango huu wa kushirikiana na wakulima kuwa utaweza kuinua sekta ya
kilimo nchini kwa haraka na kuboresha maisha ya wakulima.
Huu ni mfano wa uwekezaji
wenye faida kwa watanzania kwa kuwa unaeleta mabadiliko kwenye jamii na
kubadilisha maisha ya wananchi wengi kuwa bora.
0 comments:
Post a Comment