Nafasi Ya Matangazo

April 21, 2016

 Mfungaji wa CDA Dodoma, Tatu Fungo akiuwahi mpira katika mchezo wao wa netiboli wa Kombe la Mei dhidi ya Uchukuzi SC. Uchukuzi walishinda kwa magoli 23-16.
Mchezaji Mwadawa Hamisi wa Uchukuzi SC (GK) akiangalia mwenzake wa kumrushia baada ya Tatu Fungo wa CDA kufunga bao katika michuano ya Mei Mosi. Uchukuzi walishinda magoli 23-16.
Mchezaji Matalena Mhagama wa Uchukuzi SC (GS) akijiandaa kupokea mpira kutoka kwa Tatu Kitula aliyezuiwa na Catherine Ukunguala, katika mchezo wa netiboli wa mashindano ya Mei Mosi.
*****************
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TIMU ya netiboli ya Uchukuzi SC jana ilianza vyema mchezo wake wa kwanza kwa kuwaicharaza CDA ya Dodoma katika mashindano ya Mei Mosi yanayoendelea mkoani Dodoma.

Uchukuzi SC inayoundwa na wachezaji wakongwe, akiwemo mfungaji mahiri wa timu ya Bandari na Taifa, Matalena Mhagama waliwapeleka puta wapinzani wao ambapo hadi mapumziko walikuwa mbele kwa magoli 11-6.

Katika mchezo huo uliokuwa umetawaliwa na rafu za hapa na pale na kulalamikiwa mara kwa mara na wachezaji wa Uchukuzi SC, ulimalizika kwa mfungaji Matalena kufunga magoli 16 na Tatu Kitula akifunga saba, wakati wapinzani wao Tatu Fungo nma Margeth Nicholaus kila mmoja akifunga magoli nane.

Kocha Mkuu wa Uchukuzi SC, Judith Ilunda alisema wamepata ushindi huo wa kwanza kutokana na kufanya mazoezi ya pamoja ya muda mrefu, pamoja na kwamba wapinzani wao walikuwa ni wazuri na wenye uzoefu mkubwa.

“Wengi waliocheza na kikosi change ni wakongwe wapo niliocheza nao mimi kwenye mashindano mbalimbali, hivyo wameweza kutumia ukongwe wao lakini tuliwazidi mbinu kutokana na timu yetu kuundwa na chipukizi wengi,” alisema Ilunda.

Lakini, alilalamikia maamuzi ya waamuzi waliocheza mchezo huo kuwa mengi yamepitwa na wakati kutokana na sheria kubadilika mara kwa mara.

“Hawa waamuzi wamekuwa wakichezeshakwa sheria nyingi za zamani na kusababisha mvutano, hivyo wanatakiwa wabadilike kwa kujisomea mara kwa mara ili kuondoa mkanganyiko kwa timu zinazocheza,” alisema Ilunda.

Hatahivyo, waamuzi Mariam Makisi na Caroline Paulo wote wa Dodoma, kwa nyakati tofauti walisema wamechezesha mchezo huo kwa kanuni na sheria za mchezo huo, lakini wameshangazwa na malalamiko ya kuwa wamechezesha kwa sheria za zamani.

“Unajua timu za Dar es Salaam siku zote zinajifanya kujua sheria zaidi, na wangeweka wazi ni wapi waamuzi tulipopindisha sheria,” alisema  Makisi.

Wakatihuohuo, timu ya Tamisemi iliwafunga TPDC kwa magoli 6-1 katika mchezo wa soka uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri.

Wafungaji wa Tamisemi ni Mwigane Yeya kafunga magoli mawili, wakati waliofunga moja-moja ni Hamis Shedafa, Hamad Majura, Nelson Richard na Phillipo Oden; wakati bao la kufutia machozi la TPDC lilifungwa na Shija Dalushi.

Katika mchezo mwingine wa soka, timu ya Tanesco ilipata ushindi wa chee baada ya wapinzani wa CWT ya Dodoma kushindw kutokea uwanjani.
Posted by MROKI On Thursday, April 21, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo