Nafasi Ya Matangazo

November 05, 2015

UFAULU wa watahiniwa wa mitihani ya shule ya msingi kwa mwaka 2015, umepanda kwa asilimia 10.85 huku shule za Kanda ya Ziwa zikifanya vizuri zaidi. Akitangaza matokeo hayo jana, Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alisema watahiniwa 518,034 kati ya watahiniwa 763,602, waliofanya mitihani yao mwaka 2015 wamefaulu kwa kupata alama 100 na zaidi kati ya alama 250, ambayo ni asilimia 67.84.


Mwaka 2014 watahiniwa 451,392, kati ya watahiniwa 792,118 waliofanya mitihani walifahulu mitihani yao, ambayo ni asilimia 56.99, hivyo kuwa na ongezeko la ufaulu kwa asilimia 10.85. Alisema kati ya hao, watahiniwa 264,130 ni wasichana ambao ni asilimia 64.60 na wavulana ni 253,900 ambao ni asilimia 71.58.


Akitoa mchanganuo wa ufaulu katika madaraja, Dk Msonde alisema waliopata daraja A ni watahiniwa 25,663 (asilimia 3.36), daraja B ni 155,071 (asilimia 20.31), daraja C ni 337,300. Kundi hilo lenye ufaulu wa daraja A, B na C kwa mujibu wa Dk Msonde, ndilo lenye uhakika wa kuendelea na elimu ya kidato cha kwanza.  KUONA MATOKEO YAKO BOFYA HAPA
Watahiniwa waliopata daraja D ni 224,837 (asilimia 29.44) na daraja E ni 20,731 (asilimia 2.71), ambao ndio waliofeli mitihani yao. Kiingereza kigumu Akitoa mchanganuo wa ufaulu wa kimasomo, Dk Msonde alisema ufaulu katika masomo umepanda kwa asilimia kati ya 4.61 na 17.22 ikilinganishwa na mwaka 2014.


Alisema watahiniwa wamefaulu zaidi katika somo la Kiswahili kwa asilimia 77.20 ambapo ni watahiniwa 589,425 na somo walilofaulu kwa kiwango cha chini zaidi ni Kiingereza kwa asilimia 4.14 ambapo ni watahiniwa 370,726 tu waliofanya vizuri somo hilo.


Watahiniwa 472,939 wamefanya vizuri somo la Maarifa, Hisabati ni watahiniwa 378,505 na sayansi ni watahiniwa 550,486.“ Baraza limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa wanne, ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa baadhi ya masomo.


Watahiniwa hao watapewa fursa ya kurudia mtihani mwaka 2016,” alisema. Wanafunzi 10 bora Akizungumzia watahiniwa bora kitaifa, Msonde aliwataja na shule zao kwenye mabano kuwa ni Jaffar Matange na Karim Seyn (Hazina-Dar es Salaam), Teddy Range, Paulina Gervas, Nyegoro Amos, Juster Mgarula na Janet George (Mugini-Mwanza), Ibrahim Kondo (Rocken Hill-Shinyanga), Godbless Hhayumana na David Mtalemwa (Twibhoki-Mara).


Aliwataja watahiniwa 10 bora wasichana kuwa ni Teddy Range, Paulina Gervas, Nyegoro Amos, Juster Mgarula, Janet George, Rachel Masanja na Perine Kandisso (Mugini), Irene Michael na Happiness Chacha (Twibhoki) na Philimina Philimatus (Little Flower).


Watahiniwa 10 wa kiume ni Jaffar Matange na Karimu Seyn (Hazina), Ibrahim Kondo (Rocken Hill), Godbless Hhayuma na David Mtalemwa (Twibhoki), Ismail Sigera na Rajab Mohammed (Hazina), Henry Chamatata (Rocken Hill), Kelvin Joseph (Little Flower) na Gemystone Thompson (Rocken Hill).


Shule bora Dk Msonde alitaja shule zilizofanya vizuri kuwa ni Waja Springs (Geita), Enyamai na Twibhoki (Mara), Mugini (Mwanza), Rocken Hill (Shinyanga), Karume (Kagera), Alliance (Mwanza), Little Flower (Mara), Palikas (Shinyanga) na St. Caroli (Mwanza).


Alitaja shule zilizofanya vibaya kuwa ni Mwashigini (Shinyanga), Mabambasi (Simiyu), Mwangu (Lindi), Mohedagew (Arusha), Kwale (Pwani), Njoro (Arusha), Gomhungile (Dodoma), Makole (Tanga), Kitengu na Koloni (Morogoro).


Pia Msonde alitaja mikoa iliyofanya vizuri kuwa ni Katavi, Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Geita, Kagera, Tanga, Njombe na Iringa. Kwa upande wa halmashauri zilizofanya vizuri ni Mpanda Mji (Katavi), Arusha Mjini (Arusha), Biharamulo (Kagera), Hai (Kilimanjaro), Ukerewe (Mwanza), Korogwe Mjini (Tanga), Arusha (Arusha), Moshi Mjini (Kilimanjaro), Kinondoni (Dar es Salaam) na Ilemela (Mwanza). Source:Habarileo online

Posted by MROKI On Thursday, November 05, 2015 1 comment

1 comment:

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo