Nafasi Ya Matangazo

April 09, 2015

Viongozi Wapya waliochaguliwa katika Mkutano Mkuu wakiwa katika picha ya pamoja ikiwa ni kumbukumbu ya Uchaguzi huo.
Wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma Beijing China wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa Jumuiya hiyo na kuwapata Viongozi wapya baada ya kuchagulia kwa kuongoza Jumuiya hiyo kwa mwaka 2015/2016.
************
Na Father Kidevu Blog, Beijing 
VIONGOZI wapya wa Jumuiya ya Wanafunzi Watanzania wa Vyuo Beijing (TZ-SUB) umeahidi kuendeleza mshikamano na kusimamia misingi ya uzalendo kwa Taifa katika kipindi chao cha uongozi cha mwaka mmoja.

Walisema kwa nyakati tofauti kuwa, Tanzania ni nchi yenye misingi ya undugu na umoja ambao umefanya watu kuishi kama watoto wa familia moja tangu enzi na enzi hivyo misingi hiyo wataisimamia ugenini ili kudumisha umoja wa Taifa. 

Viongozi hao wapya walichaguliwa mwanzoni mwa wiki katika Mkutano Mkuu wa TZ-SUB uliofanyika katika Ukumbi wa Ubalozini mjini hapa na kuhudhuriwa na Balozi wa Tanzania, China, Abdulrahman Shimbo pamoja na Mwambata wa Elimu, George Manongi. 

Uchaguzi wa viongozi hao uliosimamiwa na kuandaliwa na Kamati Tendaji, Tume ya Uchaguzi ya Umoja na Ubalozi. Waliochaguliwa na nafasi zao katika mabano ni Ireneus Kagashe (Mwenyekiti), Mbarak Abdulrahman Said (Makamu Mwenyekiti), Godfrey Steven (Katibu Mkuu), Asha Hijja Khamis (Naibu Katibu Mkuu) na Ezekiel Dembere (Mweka Hazina). 

Mwenyekiti mpya, Kagashe aliwaambia wanachama wa TZ-SUB kuwa, pasipo ushirikiano wa karibu, umoja huo hauwezi kuleta matunda na kuwataka wanachama kuwapa ushirikiano kama walivyokuwa wakifanya kwa viongozi waliomaliza muda wao. 

“Tunategemea kufanya kazi na ninyi, bila ushirikiano wenu hatuwezi kutimiza malengo ya umoja, hivyo nyie ndio mnaotutuma kazi na kushirikiana nasi kufikia malengo, naomba tushirikiane kwa karibu, kuelekezana na kukosoana kwa staha pale inapotakiwa,” alisema Kagashe. 

Akizungumza kabla ya Uchaguzi huo, Balozi Shimbo aliwataka wanavyuo na hasa viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza wenzao kusimamia umoja wa nchi na kusisitiza kupelea utaalamu nyumbani pindi wanapomaliza masomo yao kwani Taifa linawasubiri na kuwategemea. 

“Umoja ni nguvu, tuwe wamoja na tuuendeleze umoja huo, vijana ni Taifa la leo, uaminifu na uadilifu ni kitu muhimu, kuna mataifa umoja kama huu umekuwa vigumu kwasababu wameingiza tofauti zao za kivyama, huu ni umoja wa Watanzania, si vinginevyo,” alisema Balozi Shimbo. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Suleiman Serera, alimuhakikishia Balozi kuwa, umoja huo utaendelea kushirikiana na serikali kuongeza kasi ya maendeleo nyumbani na kwamba lengo kuu hilo litafikiwa kwa kusimamia umoja, ushirikiano na uzalendo. 

Serera pia aliipongeza Tume ya Uchaguzi ya TZ-SUB chini ya Mwenyekiti wake Damas Cosmas kwa kuandaa uchaguzi kwa misingi ya demokrasia, sheria na kanuni jambo lililotoa nafasi kila mwananchama kutumia haki yake ya kupiga na kupigiwa kura.
Posted by MROKI On Thursday, April 09, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo