Nafasi Ya Matangazo

June 11, 2013

 Dk. Mwelecele Malecela-Mkurugenzi wa NIMR


Hussein Makame –MAELEZO

SERIKALI imewaomba wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza wenye umri kuanzia miaka mitano na kuendelea kujitokeza kwa wingi katika zoezi la umezaji wa dawa za Matende na  Mabusha(Ngirimaji),na Kichocho litakalofanyika kuanzia Juni 22 hadi na Agosti mwaka huu.

Wito huo umetolewa na Afisa Mradi wa   Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD), Bernad Kilembe katika mafunzo kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari juu ya mpango huo yaliyofanyika ofisi za NIMR  jijini Dar es Salaam leo.

Alisema zoezi hilo linatarajiwa kufanyika katika majiji  hayo  kuanzia Juni 22  hadi 26 mwaka huu na litakuwahusisha wakazi wote wa maeneo hayo, ambapo watameza dawa za ALBENDAZOLE na MECTIZAN kwa Dar es Salaam na PRAZIQUANTEL kwa Mwanza.

Alisema zoezi hilo litafanyika katika vituo 1500 vilivyoko jijini Dar es Salaam ambapo kwa upande wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano watameza dawa ya PRAZIQUANTEL kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa kichocho.

Alivitaja vituo hivyo kuwa ni shule za msingi, vituo vya mabasi,sokoni, magerezani, taasisi mbalimbali, maofisini na kambi za jeshi.

Alisisitiza kuwa kwa upande wa watoto wanatakiwa wameze dawa ya PRAZIQUANTEL masaa mawili baada ya kula, ambapo kwa mkoa wa Mwanza zoezi litahusisha umezaji wa dawa hiyo kwenye shule za msingi kwa watoto wenye umri wa kwenda shule za msingi mwezi wa Agosti, mwaka huu.

Akizungumzia ugonjwa Matende na Mabusha,Kilembe alisema maambukizi ya magonjwa hayo na kichochco yameenea karibu nchi nzima ambapo alisema tatizo hilo lipo kwa kiwango cha kuanzia asilimia 1 hadi 69.

Akizungumzia zoezi hilo, Afisa Mradi wa NTD, Dk.Edward Kirumbi aliwataka wananchi wa majiji hayo kuondoa hofu juu ya dawa hizo kwa kuwa hazina athari huku akikanusha uvumi kuwa ukipasuliwa ngirimaji utakufa au itaathiri nguvu za kiume.

Naye Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Neema Rusaibamayila aliwataka wahariri hao kufikisha ujumbe kwa jamii na kuwahamasiaha wananchi kuhudhuria kwenye zoezi hilo.

Mpango huo unahusisha udhibiti wa magonjwa matano ,ambayo ni Matende na Mabusha(Ngirimaji), Magonjwa mengine ni Usubi, Trakoma na Minyoo ya Tumbo.

 Alisema  ugonjwa wa  Matende na Mabusha husababishwa na minyoo midogo,huenezwa na mbu aina ya Culex na Anopheles, wakati ugonjwa wa kichocho husababishwa na minyoo jamii ya Schistosoma.
Posted by MROKI On Tuesday, June 11, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo