Nafasi Ya Matangazo

July 18, 2009

Mwandishi wa Habari Leo afariki dunia, ni Makubo Haruni.
Na Nashon Kennedy,Mwanza

MWANDISHI wa habari mwakilishi wa gazeti hili wa mkoa wa Mara, Makubo Haruni (45), amefariki dunia.

Haruni alifikwa na mauti majira ya saa tatu, usiku wa kuamkia jana, wakati akiwa njiani kupelekwa kutibiwa katika Hospitali ya Dk. Winani, iliyopo mjini Tarime.

Kwa mujibu wa kijana mkubwa wa Haruni, Marwa Makubo, akizungumza kwa njia ya simu kutoka Tarime alisema kuwa marehemu baba yake alirejea nyumbani Mtaa wa Songambele, majira ya saa mbili usiku juzi na kwamba baada ya dakika chache alianza kulalamika kuwa anajisikia moyo unampasuka.


“Baba alifika akiwa na hali isiyokuwa ya kawaida na baadaye akaanza kulalamika kuwa moyo unapasuka,” alisema Marwa.


Aliongeza kuwa alimsogelea na kuanza kumpukutishia upepo kwa kutumia nguo, lakini marehemu aliishiwa nguvu, na ndipo akasaidiana na majirani kumkimbiza hosipitalini ambapo hata hivyo mganga wa zamu aligundua kuwa alikuwa ameishakata roho.

Marwa alisema kwamba siku nne kabla ya kifo cha baba yake , alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa malaria, lakini kufikia juzi alikuwa amepata nafuu baada ya kutumia dawa.

Kaka wa Haruni, Mussa Haruni, aliliambia gazeti hili kuwa mwili wa marehemu ambao jana ulikuwa unahifadhiwa chumba cha maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, utasafirishwa kwenda kijijini Muriba kwa mazishi baada ya taratibu za mazishi kukamilika.


Marehemu makubo alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Muriba, wilayani Tarime na baadaye katika Shule ya Sekondari ya Ikizu, wilayani Bunda, mkoani Mara. Ameacha mke na watoto wanne.
MWISHO.
Posted by MROKI On Saturday, July 18, 2009 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo