Mkurugenzi wa Leseni wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza
Swedi, amewataka wamiliki wa leseni, mameneja na wakaguzi wa migodi kujiandaa
mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, kwa
lengo la kulinda maisha ya watu, mazingira, miundombinu na kuhakikisha shughuli
za uzalishaji migodini zinaendelea kwa usalama.
Mhandisi Swedi ametoa agizo hilo wakati akifunga mafunzo
yaliyowakutanisha washiriki 510 mjini Kahama, kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa
Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, akisisitiza kuwa maandalizi ya
kukabiliana na mvua hizo yanapaswa kuzingatia hali halisi na vihatarishi
vilivyopo katika kila mgodi.
Amesema washiriki wanapaswa kutekeleza maelekezo
yaliyotolewa katika mafunzo hayo na kutumia maarifa waliyoyapata katika maeneo
yao ya kazi ili kuzuia na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua
hizo, ambazo zimetabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
Kwa mujibu wa Mhandisi Swedi, mafunzo hayo yalilenga
kuongeza uelewa na utayari wa wamiliki wa leseni, mameneja na wakaguzi wa
migodi katika kujiandaa, kuzuia na kukabiliana na maafa yanayoweza kujitokeza
kutokana na mvua kubwa, pamoja na kulinda miundombinu ya uchimbaji.
Amesema mada zilizowasilishwa zilihusu maandalizi ya
kukabiliana na maafa, maeneo na miundombinu ya migodi inayoweza kuathirika,
wajibu wa mameneja na wakaguzi wa migodi, pamoja na taratibu sahihi za
uchimbaji na namna ya kuhakikisha usalama na uimara wa miamba.
Amewataka washiriki kuhakikisha taratibu za kiutendaji na
ukaguzi zinaandaliwa na kutekelezwa ipasavyo, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara
wa maeneo na miundombinu ya migodi na kubaini vihatarishi mapema kabla
havijasababisha madhara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na
Mazingira, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema Tume ya Madini itaendelea
kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ukaguzi wa migodi, ikiwemo kusambaza
vifaa vya kisasa vya ukaguzi katika mikoa ya kimadini.
Amesema hatua hiyo inalenga kurahisisha ukaguzi na kusaidia
kubaini hali ya maeneo ya chini ya ardhi, huku akiwataka wachimbaji wadogo
kuimarisha usalama kwa kutengeneza kanuni ndogo na kufanya vikao kabla ya
kuanza kwa kila zamu ili kubaini idadi ya watu wanaoingia migodini.
Mhandisi Kamando amesisitiza kuwa wakati wa mvua, watu
hawapaswi kuruhusiwa kuingia katika mashimo yenye vihatarishi vya usalama.
“Wakaguzi wa madini, kama kuna kipindi hamtakiwi kulala ni
hiki. Kama duara ni bovu, msioneane haya kusema ukweli. Mmiliki wa duara
akikaidi na kupeleka watu, hatua stahiki zichukuliwe,” amesema Mhandisi Kamando.
Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Tume ya Madini,
Francis Kayichile, aliwataka wachimbaji kuzingatia sheria, kanuni na masharti
ya leseni zao, akieleza kuwa kila leseni ya uchimbaji ina masharti ambayo
mwenye leseni anatakiwa kuyatekeleza.
“Shimo likipata shida wakati mlishatahadharishwa, sheria
itawabana na hatutafumbia macho,” amesema Kayichile.



.jpeg)





0 comments:
Post a Comment