Nafasi Ya Matangazo

August 01, 2026






Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam
Kufuatia mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Mamkala ya Mapato Tanzania (TRA), imetoa elimu na mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara na walipakodi ili kuwa na uelewa wa pamoja wa masuala ya kodi.

Mafunzo hayo yameratibiwa na TRA mkoa wa kikodi wa Kariakoo, Julai 30, 2026, Jijini Dar es Salaam.

Katika mafunzo hayo, Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, CPA Paul Walalaze, amesema miongoni mwa mabadiliko ya sheria za kodi ni pamoja kutoa msamaha wa kodi kwa muda wa miezi 12 (mwaka mmoja) kwa mfanyabiashara mpya ambaye mauzo yake kwa mwaka hayazidi shilingi milioni 200.

"Serikali imesikia kilio cha wafanyabiashara wapya ambao wanaanza bishara zao. Katika mabadiliko haya, mfanyabiashara mdogo anayeanza biashara ambaye mauzo yake kwa mwaka hayazidi shilingi millioni 200, atapata msamaha wa kodi katika kipindi cha miezi 12 tangu aliposajiliwa," amesema Walalaze.

Aidha, amesema mfanyabiashara anapoanza kufanya shughuli zake za biashara, anahitaji kujijenga kabla ya kuanza kulipa kodi, hivyo, wafanyabiashara na wajasiriamali wanapaswa kuchangamkia fursa hii kwa kuanzisha biashara kwani wana kipindi cha neema (grace period) cha kujijenga kibiashara kabla ya kuanza kulipa kodi.

Katika hatua nyingine, Walalaze amekumbusha umuhimu wa kufanya miamala ya malipo kwa njia ya kieletroniki ili kuwezesha malipo hayo kufika panapohusika na hivyo kuchangia makusanyo ya kodi.

"Sheria ya Miamala ya Kieletroniki inahimiza malipo yote kama vile ya ununuzi wa mashamba, nyumba, magari, ada za shule, huduma za migahawa na mengineyo, kufanyika kwa njia ya kieletroniki," amesema.

Halikadhalika, Walalaze amewajuza wafanyabiashara hao kuwa, Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inamtaka wakala wa kodi ya zuio kuwasilisha na kufanya malipo ya VAT alizozuia ndani ya siku kumi ya mwezi unaofuata.

Kimsingi, serikali kupitia TRA, katika utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027, imefanya mabadiliko ya sheria nyingi za kodi ambapo sasa wanao wajibu wa kutoa elimu kuhusiana na mabadiliko hayo kwa wafanyabiashara, walipakodi na wananchi kwa ujumla.

Awali, akizungumza kuhusiana na mafunzo hayo, Kaimu Meneja Msaidizi wa Huduma kwa Walipakodi, Khalid Mchuma, amesema wafanyabiashara wayatumie mafunzo hayo katika utendajikazi wao wa kila siku ili kuendelea kujenga nchi kupitia ulipaji kodi wa hiari na kwa moyo wa uzalendo.
Posted by MROKI On Saturday, August 01, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo