Nafasi Ya Matangazo

July 25, 2026







Bukombe, Geita
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameendelea na ziara yake ya kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Geita kwa kutembelea miradi mbalimbali katika Wilaya ya Bukombe, huku akisisitiza umuhimu wa kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma zinazotarajiwa.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara, Waziri Mavunde amesema serikali chini ya uongozi wa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan  imedhamiria kuleta miradi mingi ya maendeleo ili kupeleka huduma za msingi kwa wananchi.


Awali, Waziri Mavunde alikagua mradi wa maji katika Kijiji cha Businda, Kata ya Bulangwa, wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 963.7. Mradi huo unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 9,949 na kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama katika eneo hilo.

Katika ziara hiyo, Mhe. Mavunde ametembelea na kukagua ujenzi wa soko na standi kuu ya kisasa ya mabasi katika Kata ya Katente, Ushirombo, mradi wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 22 na kumpongeza Mbunge wa Bukombe Mh. Dkt. Doto M. Biteko kwa kusaidia upatikanaji wa miradi hii ya kimkakati kupitia serikali kuu na pia kutoa rai kwa mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji ili mradi ukamilike kwa wakati na kuwawezesha wananchi, hususan waliopisha ujenzi wa mradi huo, kurejea katika shughuli zao za kiuchumi.

Wachimbaji wadogo wa Bukombe wamemshukuru Rais Mh. Dkt. Samia S. Hassan kwa kuweka mazingira rafiki ya uchimbaji na kuruhusu ufutwaji wa Leseni kubwa za madini na kupewa wachimbaji wadogo.


Aidha Waziri Mavunde ametoa katazo kwa  wachimbaji wadogo kuvamia maeneo yenye leseni za utafiti na kuagiza kufuatwa kwa sheria na taratibu zilizowekwa ili kuepusha migogoro na ugumu wa usimamizi wa leseni za madini,kwa kuwa serikali sasa inaweka mpango mzuri wa ugawaji wa Leseni kwa wananchi wake.

Waziri Mavunde amekagua ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami nyepesi yenye urefu wa kilomita 1.2 kutoka Uyovu hadi Namonge katika Kata ya Runzewe, mradi unaogharimu zaidi ya Shilingi milioni 917.6. Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea biashara, kuboresha usafiri na kuongeza usalama wa wananchi wakati wa mchana na usiku.

Katika eneo la machimbo ya Msasa, Waziri Mavunde pia amekagua ujenzi wa kituo cha polisi na zahanati vinavyojengwa kwa ufadhili wa wachimbaji wadogo kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR). Amepongeza wachimbaji hao kwa kurejesha sehemu ya faida wanazopata kwa kuwekeza katika huduma muhimu za kijamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, amesema miradi inayotekelezwa katika Wilaya ya Bukombe ni mkombozi kwa wananchi na itachochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.

Shigella pia amemuomba Waziri Mavunde kumfikishia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan salamu za shukrani kutoka kwa wananchi wa Bukombe kwa kutoa fedha za ujenzi wa soko la kisasa la Ushirombo.

Amesema kukamilika kwa soko hilo kutatoa mazingira bora ya biashara, kuongeza mapato ya wananchi na Halmashauri, pamoja na kuhudumia wakazi wa Ushirombo na maeneo jirani.
Posted by MROKI On Saturday, July 25, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo