Katika kuhakikisha usafi wa
mazingira unaimarishwa nchini, Serikali imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika
sekta ya usimamizi wa taka hususan taka ozo zinazozalishwa katika vyanzo mbalimbali
kama hoteli, masokoni na majumbani.
Akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo Juni 09, 2026, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa amesema hadi kufikia Aprili, 2026 jumla ya viwanda sita vimeanzishwa kwa ajili ya kuchakata na kurejelesha taka ozo.
Mhe. Reuben Kwagilwa amesema katika kufanikisha hatua hiyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimeendelea kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya uhifadhi wa mazingira ikiwemo udhibiti wa taka.
Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Kwagilwa alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi mwanachama wa Mikataba mbalimbali ya kuhifadhi mazingira na mabadiliko ya tabinchi ambapo kupitia mikataba hii, Tanzania imekuwa ikishiriki katika mikutano ya Kimataifa ya Nchi Wanachama (COP).
Alifafanua kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Taka wa miaka mitano (2025 – 2030) wenye lengo la kuimarisha mfumo wa usimamizi wa taka kwa dhana ya uchumi rejeshi ambapo taka zinazozalishwa zinaweza kutumika tena kama malighafi viwandani.
Aidha, Mhe. Kwagilwa alilieleza Bunge kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi mwanachama wa Mikataba mbalimbali ya kuhifadhi mazingira na mabadiliko ya tabinchi ambapo kupitia mikataba hii, Tanzania imekuwa ikishiriki katika mikutano ya Kimataifa ya Nchi wanachama (COP).
Alisema kuwa kupitia mikutano hiyo ya kimataifa, Tanzania imeendelea kuchangamkia fursa kwa kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya uhifadhi wa mazingira ikiwemo udhibiti wa taka zinazozalishwa katika maeneo mbalimbali nchini hatua inayosaidia pia kusafisha mazingira.
Sanjari na hilo, aliongeza kuwa kupitia makubaliano ya Paris, Tanzania imeandaa Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Nationally Determined Contribution, NDC) ambao umebadilisha eneo la udhibiti wa taka kama mojawapo ya vipaumbele vya kupunguza uzalishaji wa hewa ya Kaboni.
Kadhalika, Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa SJMT na SMZ pia zinashirikiana katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwenye taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 ikiwemo ya gesi ili kuachana na kuni na mkaa ambao unatokana na ukataji wa miti kwa wingi.






0 comments:
Post a Comment