Nafasi Ya Matangazo

May 04, 2026

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Moses Manumbu akisikiliza mapigo ya moyo ya mwananchi aliyefika katika banda la JKCI Dar Group kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya wakati wa maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyomalizika hivi karibuni Mkoani Njombe. Jumla ya watu 386 wamefanyiwa uchunguzi wa afya katika maonesho hayo.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mahawa Asenga akimpima shinikizo la damu na mapigo ya moyo mwananchi aliyefika katika banda la JKCI Dar Group kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya wakati wa maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyomalizika hivi karibuni  Mkoani Njombe. Jumla ya watu 386 wamefanyiwa uchunguzi wa afya katika maonesho hayo.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Happiness Shirima akitoa elimu ya mtindo  bora wa maisha kujilinda na magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe waliofika katika banda la JKCI Dar Group kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya wakati wa maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyomalizika hivi karibuni Mkoani Njombe. Jumla ya watu 386 wamefanyiwa uchunguzi wa afya katika maonesho hayo.Picha na: JKCI
************
Na Mwandishi Maalumu – Njombe
Jumla ya watu 386 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi wa afya iliyofanywa  na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group.
Kambi hiyo ya siku sita ilifanyika kwenye maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyomalizika hivi karibuni katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema Mkoani Njombe.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuhitimisha kambi hiyo daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Moses Manumbu alisema kati ya watu 386 waliowahudumia 158 wamekutwa na matatizo mbalimbali ya moyo na kupewa rufaa kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.
“Baada ya kuwafanyia vipimo tumebaini watu wengi kuwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu bila ya wao kujua lakini pia wengine tumewakuta na matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo na matatizo ya mishipa ya damu kuziba hivyo kuwapa rufaa kwaajili ya matibabu zaidi”, alisema Dkt. Moses.
Mtaalamu huyo wa magonjwa ya moyo alisema kwa upande wa watoto waliowahudumia waliwakuta na na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio  wake na ugonjwa wa moyo unaosababishwa na bakteria wanaoshambulia valvu za moyo (Rheumatic Heart Diseases).
“Tunaendelea kuihamasisha jamii kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kujali afya zao kwani afya ndio mtaji wa maendelea, tukiwa na afya bora tutakuwa na uwezo wa kufanya kazi na kupata maendeleo”, alisema Dkt. Moses.
Kwa upande wake Bernadetha Kindu aliyefanyiwa uchunguzi wa afya katika banda la JKCI Dar Group alisema amekuwa akisumbuliwa na maumivu makali ya kichwa kwa muda mrefu bila ya kujua kama maumivu hayo ni dalili ya kuwa na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu.
“Nawashauri wananchi wenzangu tukiona dalili zozote za ugonjwa tufike katika vituo vya afya kufanya uchunguzi, mimi nilichukulia kawaida na kutumia dawa bila ya ushauri wa daktari jambo ambalo halikuwa salama kwa afya yangu”, alisema Bernadetha.
Bernadetha alisema baada ya kuonana na daktari ameambiwa kuwa kutumia dawa bila kufanya uchunguzi wa afya kungeweza kumletea madhara makubwa kiafya lakini pia kuhatarisha maisha yake.
Naye Kazinja Ngoyai mkazi wa Songea alisema imekuwa rahisi kwake kufuata huduma bingwa bobezi za moyo katika Mkoa wa Njombe tofauti na angezifuata Dar es Salaam ingemgharimu na kuchukua muda wake mwingi.
“Tunaposikia fursa kama hizi tusiziache zipite, mfano mzuri ni mimi nimetumia masaa machache kutoka Songea hadi hapa kuja kupima moyo wangu lakini pia nimetumia gharama ndogo ya usafiri tofauti na ningezifuata Dar es Salaam”, alisema Ngoyai.
Posted by MROKI On Monday, May 04, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo