Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa JKCI Dkt. Tatizo Waane wakizungumza na mmoja wa mashabiki wa timu ya Simba wakati wa upimaji wa magonjwa ya moyo uliofanywa na Taasisi hiyo kabla ya mechi ya mpira wa miguu baina ya mashabiki wa timu za Simba na Yanga jana katika Uwanja wa mpira wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dotto Sebastian akimsikiliza mwananchi alifika katika banda la Taasisi hiyo wakati wa kambi maalumu ya uchuguzi na matibabu ya moyo kwa mashabiki wa timu za mpira za Simba na Yanga kabla ya kuanza kwa mechi yao jana katika Uwanja wa mpira wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na baadhi ya wananchi waliojitokeza kupima moyo wakati wa kambi maalumu iliyofanywa na Taasisi hiyo jana kabla ya mechi ya mpira wa miguu kati ya mashabiki wa timu za Simba na Yanga iliyofanyika katika uwanja wa mpira wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Morris Budotela akimshauri mwananchi aliyefika kupata huduma katika kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo kabla ya kuanza kwa mechi ya mpira wa miguu baina ya mashabiki wa timu za Simba na Yanga jana katika Uwanja wa mpira wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Bruno Selege akimpima wingi wa sukari kwenye damu mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo kabla ya kuanza kwa mechi ya mpira wa miguu baina ya mashabiki wa timu za Simba na Yanga jana katika Uwanja wa mpira wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari akimfafanulia mwananchi kuhusu magonjwa ya moyo mara baada ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalumu iliyofanywa na Taasisi hiyo kabla ya kuanza kwa mechi ya mpira wa miguu baina ya mashabiki wa timu za Simba na Yanga jana katika Uwanja wa mpira wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Magreth Justine akimpima mapigo ya moyo mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa na JKCI kabla ya kuanza kwa mechi ya mpira wa miguu baina ya mashabiki wa timu za Simba na Yanga jana katika Uwanja wa mpira wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Mtaalamu wa vipimo vya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Emily Joseph akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mwananchi aliyefika katika banda la JKCI kabla ya kuanza kwa mechi ya mpira wa mashabiki wa timu za Simba na Yanga jana katika Uwanja wa mpira wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ester Paschal akimpima uwiano baina ya urefu na uzito shabiki wa Simba wakati wa kambi maalumu ya uchuguzi na matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa na JKCI kwa mashabiki wa timu za mpira za Simba na Yanga kabla ya kuanza kwa mechi yao jana katika Uwanja wa mpira wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
****************
Mwandishi Maalumu – Dar es SalaamJumla ya mashabiki 175 wa timu za Simba na Yanga wamepata fursa ya kupimwa na kutibiwa magonjwa ya moyo katika kambi maalumu iliyoendeshwa na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Kambi hiyo ilifanyika jana sambamba na mechi ya mashabiki wa timu hizo katika Uwanja wa Mpira wa Miguu wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam, ambapo mashabiki walipatiwa vipimo mbalimbali vya afya ya moyo ikiwemo kupima uwiano wa urefu na uzito.
Vipimo vingine vilivyotolewa ni pamoja na kipimo cha kiwango cha sukari kwenye damu, shinikizo la damu na mapigo ya moyo, kipimo cha mfumo wa umeme wa moyo (ECG) pamoja na kipimo cha kuangalia utendaji wa moyo (ECHO).
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kambi hiyo imelenga kuwasaidia mashabiki kufuatilia afya zao za moyo huku wakiendelea kufurahia michezo wanayoipenda.
“Nimefurahi kuona washabiki wengi wa Simba na Yanga wamejitokeza kwa wingi kupima afya zao. Ninawaomba wanapopata fursa kama hizi, wazitumie vizuri ili kujitambua kiafya na kupata elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo,” alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari alisema watu 12 wamepewa rufaa ya kufika katika taasisi hiyo kwa ajili ya uchunguzi wa kina zaidi baada ya kubainika kuwa na changamoto za kiafya.
“Waliopata rufaa wapo waliobainika kuwa na shinikizo la juu la damu, huku mmoja akigundulika kuwa na ugonjwa wa kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo. Wakifika JKCI tutafanya vipimo zaidi na kuwashauri hatua sahihi za matibabu,” alisema Dkt. Janeth.
Aliongeza kuwa washiriki wote waliopimwa wamepewa elimu ya kujikinga na magonjwa ya moyo kwa kuepuka vichochezi hatarishi kama uvutaji wa sigara, matumizi ya pombe kupita kiasi, pamoja na kuzingatia lishe bora na mazoezi ya mara kwa mara.
“Wapo tuliowakuta na shinikizo la juu la damu bila wao kujijua, jambo linaloonesha umuhimu wa kupima afya mara kwa mara,” alisisitiza.
Nao mashabiki wa Simba na Yanga waliipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwafuata wananchi moja kwa moja katika maeneo ya mikusanyiko na kuwapatia huduma za uchunguzi wa afya bila usumbufu wa kufika hospitalini.
Jonas Ibrahimu, shabiki wa Simba alisema elimu aliyopata ya jinsi ya kujikinga na magonjwa ya moyo itamsaidia kubadili mtindo wa maisha kwa kuacha tabia hatarishi, kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora.
Kwa upande wake Juma Said shabiki wa Yanga, aliomba JKCI kuendeleza kambi kama hizo katika matukio mbalimbali ya michezo na maeneo mengine ya mikusanyiko huku akisema akisema hatua hiyo ina mchango mkubwa katika kuimarisha afya ya jamii na kuokoa maisha ya Watanzania.













0 comments:
Post a Comment