Mlo kamili, kupumzika na kufanya mazoezi ni miongoni mwa mambo muhimu sana katika ujenzi wa afya ya binadamu.
Kutokana na umuhimu wa masuala haya, wataalam wa afya wamekuwa walisisitiza sana binadamu kuzingatia mlo kamili, kupumzika na kufanya mazoezi ili kujenga afya bora ambayo ni msingi wa ustawi wa maisha ya binadamu yeyote.
Palipo na afya bora ndipo palipo na maendeleo, ndiyo maana Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kutaja maradhi kama adui mmojawapo wa maendeleo na hivyo akaweza mkazo wa kupambana na maradhi ili kujenga taifa lenye watu wenye afya bora.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kama wadau muhimu wa elimu hapa nchini, wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali na wadau wengine katika kuhamasisha ujenzi wa afya bora kupitia kufanya mazoezi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dk. Bill Kiwia, wakati wa mazungumzo yake na vyombo vya habari Disemba 20, 2024, alisisitiza kuwa katika kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, HESLB imeandaa mbio za hisani (HESLB Marathon) zinazotarajiwa kufanyika Februari 15, 2025 katika viwanja vya Farasi (Green Ground) Oysterbay, jijini Dar es Salaam ili kuhamasisha ufanyaji mazoezi kwa wananchi nchi nzima ili kuchochea afya bora na kuepuka magonjwa yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya moyo, figo, kisukari na shinikizo la juu la damu (presha).
Vilevile, mbio hizo zitaambatana na kukusanya fedha kwa ajili ya uboreshaji wa elimu kwa kununua vifaa vya maabara kwa shule mbili za sekondari, moja kutoka Zanzibar na nyingine Tanzania Bara.
Aidha, fedha nyingine zinatarajiwa kutumika kuboresha Kituo cha HESLB Huduma za Simu Kwa Wateja (HESLB Customer Call Centre), huku mgeni rasmi wa mbio hizo akitarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ambaye Kwa hakika ni mdau mkubwa wa sekta ya afya na elimu.
Mbio hizo za hisani zitahusisha umbali wa kilometa Tano (05), Kumi (10) na Ishirini na moja (21) ambapo kila mshiriki atachagua umbali anaotaka kukimbia ili kujenga afya yake, lakini pia kuchangia maendeleo ya elimu na utoaji wa huduma bora kwa wateja wanaohitaji huduma mbalimbali zitolewazo na HESLB.
Gharama za kujisajili ni Sh. 35,000 kwa kundi la watu kumi au zaidi, Sh. 40,000 kwa mtu mmoja na Sh.150,000 kwa watu maalum (VIP).
Zawadi kwa washindi watatu wa mbio za kilometa 21, itakuwa kama ifuatavyo; Mshindi wa kwanza atajinyakulia kitita cha shilingi milioni moja, mshindi wapili Sh. 700,000 na watatu Sh. 500,000.
Aidha, mshindi wa kwanza wa umbali wa kilometa 10 atajipatia Sh. 500,000 wapili Sh.300,000 na watatu Sh. 200,00 huku washindi watatu wa mbio za kilometa tano wakijinyakulia medali kila mmoja. Kwa maelezo zaidi namna ya kushiriki, unaweza kuwasiliana na Mratibu wa mbio hizi kwa simu namba 0754 241 241.
Ubunifu huu uliofanywa na uongozi wa HESLB kuandaa mbio hizi za hisani, ni muhimu kuungwa mkono na wananchi kwani ushiriki wa wananchi una manufaa moja kwa moja katika kuboresha elimu hasa masomo ya sayansi ambayo ni muhimu sana katika kuchagiza maendeleo nchini.
Sanjari na hilo, mbio hizi zitasaidia kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi watakaopiga simu HESLB na hivyo kuhudumiwa vyema.
0 comments:
Post a Comment