Nafasi Ya Matangazo

January 03, 2025

Wakazi wa Shehia ya Kinyikani wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba, Visiwani Zanzibar wameondokana na adha ya ukosefu wa huduma za afya baada ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Kinyikani na nyumba ya watumishi kwa gharama ya shilingi milioni 552.

Kituo hicho kimezinduliwa leo na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid ikiwa ni sehemu ya Shamrashamra za kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika tarehe 12 Januari Kisiwani Pemba.

Akizungumza baada ya kuzindua kituo hicho, Spika Maulid aliipongeza TASAF kwa kuendelea kutekeleza miradi inayolenga kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma za kijamii pamoja na kutekeleza afua za kuondoa umaskini wa kipato kwenye kaya za walengwa.

Pia aliwahimiza wananchi wa Shehia ya Kinyikani na wananchi wa Wilaya ya Wete kutunza miundombinu iliyojengwa ili kituo kiwe na tija kwa muda mrefu.

“Ninawapongeza TASAF kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na kutekeleza mpango unaojikita kwenye kuondoa umaskini, lakini, ni muhimu kwa wananchi sasa kutunza mradi huu uliojengwa kwa gharama na dhamira ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya katika eneo hili,” alisema.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Shedrack Mziray alisema katika kipindi cha Pili cha Mpango jumla ya shilingi bilioni 3.1 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miradi 15 ya kuendeleza miundombinu katika sekta ya Elimu, Afya na Maji visiwani Zanzibar.

“Katika Mamlaka ya Eneo la Utekelezaji Pemba, kwa mwaka 2024, TASAF inatekeleza jumla ya miradi 7 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.32, miradi hiyo inahusisha sekta tofauti ikiwemo afya ambayo miongoni mwa miradi yake ni ujenzi wa Kituo hiki cha Afya cha Kinyikani,”

“Aidha, miradi miwili ambayo ni Ujenzi wa Kituo cha Afya Kendwa pamoja na Madarasa katika Skuli ya Piki ilikwisha kamilika na sasa imeanza kutoa huduma kwa wananchi,” aliongeza.

Posted by MROKI On Friday, January 03, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo