Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Mpango Mahsusi
wa Kitaifa kuhusu Nishati (National Energy Compact) uliozinduliwa leo unalenga
kuiwezeseha Tanzania kuunganisha umeme kwa kaya milioni 8.3 zaidi ifikapo mwaka
2030.
Rais Dkt. Samia ameyasema
hayo wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Afrika kuhusu Nishati uliofanyika leo
katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere.
Tanzania ilikuwa mwenyeji
wa mkutano huo uliohudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Burundi, Botswana,
Congo, Comoros, Djibouti, Ethiopia, Gabon, Ghana, Guinea Bissau, Kenya,
Lesotho, Liberia, Libya, Madagascar, Malawi, Mauritania, Nigeria, Sierra Leone,
Somalia na Zambia.
Vile vile, mkutano huo
umehudhuriwa pia na Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali, Wakuu wa Mashirika
ya Fedha ya Kimataifa, Mashirika ya Kimataifa, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia
kwa lengo la kuongeza kasi ya usambazaji umeme barani Afrika ili kuwaunganisha
watu milioni 300 na umeme katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Rais Dkt. Samia
amesema kuwa kwa kutoa kipaumbele katika upatikanaji wa nishati ya umeme,
mkutano huo ulioandaliwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia na Benki ya
Maendeleo ya Afrika utawezesha kuleta mageuzi ya kiuchumi, kukua kwa viwanda,
kupunguza umaskini na kuimarisha ustawi wa watu.
Mkutano huo
umefanikiwa kupata ahadi za ufadhili wa Dola za Marekani Bilioni 40 kutoka
Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili ya kuwezesha
usambazaji wa umeme barani Afrika. Aidha, jumla ya nchi za Afrika 12 zimeingia
kwenye Mipango Mahsusi wa Kitaifa kuhusu Nishati.
Rais Dkt. Samia
amesema kuwa kupitia Mpango Mahsusi kuhusu Nishati, Tanzania inakusudia kuvutia
mitaji na uwekezaji zaidi itakayowezesha kuongeza uzalishaji wa umeme nchini na
kukukamilisha kuunganisha Mtandao wa Umeme wa Tanzania na nchi jirani ili
kuwezesha biashara ya kuuza na kununua nishati hiyo.
Mpango huo utawezesha
Serikali kukamilisha usambazaji umeme katika Vitongoji vyote 64,359 nchini ifikapo
2030. Vilevile, Mpango huo utapandisha kiwango cha uunganishaji wa umeme kutoka
46% ya sasa hadi kufikia 75%.
Vilevile, Rais Dkt.
Samia ambaye amekuwa kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ameweka
bayana kuwa Mpango huo wa Nishati pia utasaidia
kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, ikiwemo gesi asilia na
majiko banifu.
0 comments:
Post a Comment