Nafasi Ya Matangazo

July 09, 2024


Na Shamimu Nyaki
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Suleiman Serera ametoa pongezi kwa wananchi wa ndani na nje ya Tanzania waliotembelea banda la maonesho la Wizara hiyo tangu kuanza kwa maeonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam (SabaSaba) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam ili kupata elimu na huduma mbalimbali.

Dkt. Serera ametoa pongezi hizo Julai 9, 2024 alipotembelea banda la maonesho la wizara hiyo kuona namna waelemishaji wanavyotoa huduma na elimu kwa wananchi kuhusu sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.

"Nimearifiwa hapa kwamba tangu Julai 1 hadi leo Julai 9, takribani wananchi 5111 wametembelea banda letu na wapo ambao hawakujiandikisha, Banda letu limekua kivutio kwa sababu sisi ni Wizara ya furaha na tunasema "Furaha yenu ni wajibu wetu" kwa hiyo mbali na kutoa elimu na huduma pia tumewaburudisha wananchi waliotembelea maeonesho haya."

Amesema kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Kiswahili kimeendelea kukua ikiwa ni pamoja na kuandaa Kamusi kwa ajili ya shule za msingi ambayo tayari imesambazwa.

Kwa upande wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Bodi ya Filamu amewataka waendelee kuibua vipaji katika ngazi ya chini kupitia programu mbalimbali ikiwemo BASATA Vibes na Filamu Mtaa kwa Mtaa.

Aidha, amewakaribisha wananchi wajiunge na Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya pamoja na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo(TaSUBa) ili kupata elimu kuhusu Sanaa na Michezo kupitia vyuo hivyo na kuutumia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania kuomba mikopo kwa ajili ya kuendeleza kazi zao.

Dkt. Serera pia amewataka wabunifu wa kazi za Sanaa na uandishi kuhakikisha wanasajili kazi zao katika Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) pamoja na kutembelea Kituo Cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kupata Historia ya namna Tanzania iliyosaidia nchi nyingine kupata uhuru.













Posted by MROKI On Tuesday, July 09, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo