Novemba
11, 2023, Bi. Janeth (35), mkazi wa Manyoni Singida, alifika Hospitali ya
Benjamin Mkapa (BMH) baada ya kukaa siku saba katika Hospitali ya Wilaya ya
Manyoni akiimuuguza mwanaye aliyepatwa “degedege”.
Siku
hiyo, ikawa safari ya siku 60 za mtoto wake huyo mwenye umri wa miaka 4 kwenye
Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda ya
Kati.
“watu
walikuwa wanakuja, wanaruhusiwa wanamuacha mwanangu, wakati mwingine anabaki
peke yake”. alisema Bi. Janeth.
Dkt.
Venance Misago ni Bingwa wa Ganzi na Wagonjwa Mahututi, na Mkuu wa Idara ya
Huduma za Uangalizi Maalumu BMH amesema, Moyo wa mtoto huyo ulisimama ghafla
(cardiac arrest) mara nne (4) ndani ya siku 60 mtoto huyo alipokuwa ICU.
“aligundulika
kuwa na maambukizi kwenye Ubongo (meningitis), hali iliyokuwa inasababisha
apoteze fahamu mara kwa mara” alieleza Dkt. Misago.
Aidha,
Dkt. Misago amesema kuwa kwa kawaida mgonjwa hukaa katika Chumba cha uangalizi
maalumu siku 3 hadi 14 lakini maambukizi aliyokuwa nayo mtoto huyo yalisambaa
kiasi cha kusababisha presha kushuka na kupelekea Moyo kusimama (septic shock)
mara kwa mara.
Ingawa
hali hiyo haikuwa rahisi kwa Bi. Janeth, hakusita kumshukuru Mungu, Madaktari
na Wauguzi waliyomhudumia mwanaye.
“...nilipitia
wakati mgumu kiasi cha kukata tamaa, namshukuru Mungu kwa kumponya mwanangu,
nawashukuru Madaktari na wauguzi kwa kumpambania mwanangu” alieleza Bi. Janeth
kwa furaha.
Kwa
mujibu wa Awadhi Mohamed, Mkurugenzi Msaidizi huduma za Usitawi wa Jamii
Hospitali ya Benjamin Mkapa imetumia Shilingi 10, 100,000 kugharamia dawa,
vifaa tiba na chakula kwa kipindi chote cha siku 60 Mtoto wa Bi. Janeth
alipokuwa ICU.
Kupona
kwa mtoto huyo ni kielelezo cha faida za uwekezaji katika sekta ya Afya nchini,
hasa mapinduzi yanayofanywa katika kuboresha huduma za Wagonjwa Mahututi.
0 comments:
Post a Comment