Afisa Mtafiti wa Soko la Ajira Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati , Sadan Komungoma akizungumza wakati akifungua mafunzo ya ufugaji bora wa mbuzi na kondoo yaliyofanyika hivi karibuni Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma. Kulia ni Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka VETA Mkoa wa Singida, Dkt. Dickson Mkopi na kushoto ni Mwezeshaji wa mafunzo hayo Afisa Mifugo Wilaya ya Bahi, Daniel Kilogo.
***************
Na Dotto Mwaibale, Dodoma
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati imeendelea
kuunga mkono jitihada za Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia
Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanainuka kiuchumi kupitia sekta
mbalimbali ikiwemo ya ufugaji kwa kutoa mafunzo ya ufugaji bora wa mbuzi na
kondoo kwa wafugaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.
Mafunzo hayo ya ufugaji wa mbuzi na kondoo katika wilaya hiyo yamelenga kuwawezesha wafugaji kuondokana na ufugaji wa mazoea kwenda kwenye ufugaji wenye tija utakaowakwamua kiuchumi.
Afisa Mtafiti wa Soko la Ajira VETA Kanda ya Kati, Sadan Komungoma akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo hivi karibuni alisema VETA Kanda ya Kati ambayo inahusisha Mikoa ya Manyara, Dodoma na Singida wamekuwa wakifanya utafiti wa kuangalia shughuli za kiuchumi zinazofanyika kwenye maeneo husika ambapo kupitia utafiti huo wilayani humo waligundua pamoja na shughuli nyingi zinazofanyika upo pia ufugaji wa wanyama wa aina tofauti tofauti.
Alisema utafiti huo uligundua kuwa wananchi wa wilaya hiyo licha ya kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi wanajishughulisha pia na ufugaji wa mbuzi, kuku, ng’ombe na kondoo lakini wanapofuga hutumia eneo kubwa huku kukiwa na uharibifu mkubwa wa mazingira.
“Katika utafiti wetu tuligundua kuwa nchi inakuwa na maeneo mengi yamekuwa yakitumika kwa shughuli mbalimbali za uzalisha hivyo tukaona kuna haja sasa ya kuja na mafunzo ya kuwawezesha wafugaji ili waweze kufanya ufugaji mkubwa lakini katika eneo dogo,” alisema Komungoma.
Alisema kufuatia utafiti huo walioufanya Mkoa wa Dodoma hususan Wilaya ya Bahi walibaini kuwepo kwa wafugaji wengi ambao wanafuga lakini ufugaji wao hauna tija unakuta mtu anamifugo kidogo lakini anatumia eneo kubwa na kuleta changamoto kwa watu wengine ikiwa ni pamoja na mifugo yao kuingia kwenye mashamba ya wakulima na kula mazao yao.
Alisema baada ya utafiti huo wakaona wawapekee mafunzo hayo ambayo
yatawafanya watumie eneo dogo kwa ufugaji wa mifugo mingi jambo ambalo
litaisaidia Serikali kufanya shughuli zingine za maendeleo katika eneo ambalo
lingetumiwa na wafugaji wachache kama malisho ya mifugo.
“Mafunzo haya ambayo yamewahusisha wafugaji zaidi ya 58 tunaimani yataisaidia jamii na wafugaji wa wilaya hii ya Bahi kufanya ufugaji bora na wenye tija kwa kutumia eneo dogo na kuwa mabalozi kwa wananchi wengine jambo litakaloisaidia halmashauri ya wilaya katika utunzaji wa ardhi ambayo ingetumika kwa kundi moja tu la wafugaji,” alisema Komungoma.
Washiriki wa mafunzo hayo, Celina Mbete, Julius Chimwela, Stephano Petro na Mwadawa Mhando waliishukuru Serikali kupitia VETA kwa kuwapelekea mafunzo hayo ambayo yamewabadilisha kwa kuacha ufugaji wa kimazoea na kwenda kufanya ufugaji wenye tija.
“Kutokana na mafunzo haya naenda sasa kufanya ufugaji wa kibiashara ambapo nitaanza na uzalishaji wa mbuzi 20 hadi kufikisha mbuzi 244 baada ya miaka mitatu,” alisema mfugaji Julius Chimwela.
Mfugaji Celina Mbete alimshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya mafunzo ambapo alitumia nafasi hiyo kuushukuru uongozi wa VETA Kanda ya Kati chini ya Mkurugenzi wake John Mwanja na watendaji wenzake kwa kuwapa kipaumbele wafugaji wa Wilaya ya Bahi kupata mafunzo hayo.
“Binafsi nakosa cha kusema zaidi ya kumshukuru Rais wetu Mama Samia kwa kutuletea fedha hizi pia nitakuwa mchoyo wa fadhira kama sitaupongeza uongozi mzima wa VETA kwa kufanya utafiti wao na kubaini uhitaji wetu wa mafunzo haya ambayo yatatusaidia kufanya ufugaji wa wanyama kwenye eneo dogo,” alisema Mbete.
Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Chuo cha VETA Wilaya ya Bahi, Daudi Lyanga aliishukuru Serikali kwa kupeleka mafunzo hayo ambayo ni muhimu kwa jamii ya wafugaji ambapo alitumia nafasi hiyo kutangaza kozi mbalimbali zitakazoanza kutolewa katika chuo hicho kuanzia Januari 2024.
Lyanga alisema katika chuo hicho kuna kozi za muda mfupi ambazo ni ufundi wa magari, kozi ya kompyuta, ushonaji nguo, umeme wa majumbani, ufundi washi,ufundi bomba, ufundi wa kuunganisha vyuma, udereva wa bajaji na pikipiki, udereva wa awali na ujasiriamali ufugaji na kilimo.
Alisema kwa kozi za muda mrefu zitakazotolewa zitakuwa ni ya ufundi washi na kuunganisha vyuma na akawaomba vijana wa wilaya hiyo kwenda kuomba nafasi ya kuanza kozi hizo ambazo gharama yake ni ndogo.
Lyanga alisema kuwa kwa gharama za kozi hizo na namna ya kuomba nafasi hizo unaweza kuwasiliana na ofisi ya msajili wa chuo hicho kwa namba 0769-895643 au namba 0786-281937 au mwombaji kufika Chuo cha VETA Wilaya ya Bahi.
Afisa Mtafiti wa Soko la Ajira Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati , Sadan Komungoma, akisisitiza jambo kwa washiriki wa mafunzo hayo.
Kaimu Msajili wa Chuo cha VETA Wilaya ya Bahi, Daudi Lyanga, akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka VETA Mkoa wa Singida, Dkt. Dickson Mkopi. akitoa mafunzo ya ufugaji hasa katika eneo la upatikanaji wa chakula cha mifugo hiyo.
Afisa Mifugo Wilaya ya Bahi, Daniel Kilogo. akitoa mafunzo ya ufugaji bora wa mbuzi na kondoo kwa washiriki wa mafunzo hayo ambapo alifundisha aina kuu mbili za mbuzi na tabia zao ambazo ni mbuzi wa kisasa (maziwa) na mbuzi wa kawaida.
Mfugaji wa mbuzi wilayani humo, Julius Chimwela. akisisitiza jambo wakati wa mafunzo hayo.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Wafugaji wa Wilaya ya Bahi wakiwa kwenye mafunzo hayo
Mafunzo yakiendelea..
Mafunzo kwa njia ya vikundi yakifanyika.
Washiriki wakijadiliana kwa njia ya makundi wakati wa mafunzo hayo
Muonekano wa jengo la utawala la Chuo cha Ufundi VETA Wilaya ya Bahi yalipofanyika mafunzo hayo
0 comments:
Post a Comment