Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Bunju B, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko hilo pamoja na ujenzi wa Kituo cha Mabasi, Jijini Dar es Salaam, Desemba 29, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na wakazi wa Bunju B wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Soko pamoja na Kituo cha Mabasi, Bunju B jijini Dar es Salaam, Desemba 29, 2025.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na wakazi wa Bunju B wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Soko pamoja na Kituo cha Mabasi, Bunju B jijini Dar es Salaam, Desemba 29, 2025.
***************
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa maelekezo ya kuboreshwa kwa miundombinu ya Soko na Stendi ya Bunju wilayani Kinondoni ili kuwezesha wafanyabiashara na wananchi kuendesha shughuli zao kwa ufanisi na kuongeza fursa za kiuchumi katika eneo hilo.Katika ziara yake ya kikazi Bunju, Waziri Mkuu alisema soko hilo bado ni jipya na linapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia uhalisia wa biashara. Alisisitiza kuwa tozo na ushuru vinapaswa kwenda sambamba na hatua ya ukuaji wa soko.
“Hili ni soko jipya, lazima tulipe nafasi likue. Tozo na ushuru viendane na uhalisia wa biashara ili wafanyabiashara wetu waweze kuimarika na kuongeza kipato,” alisema Waziri Mkuu.
Serikali imetambua kuwa meza, vibanda na bidhaa za wafanyabiashara wadogo ndizo mitaji na ofisi zao, hivyo viongozi wa Serikali za Mitaa wameagizwa kuhakikisha wanazingatia mazingira ya soko kabla ya kutoza ushuru au kuchukua hatua zinazoweza kudhoofisha shughuli za kiuchumi za wananchi.
“Meza hizi, vibanda hivi na bidhaa hizi ndizo mitaji ya wafanyabiashara wetu. Hatuwezi kuzichukulia kama vitu vya kawaida; lazima tuzilinde,” alisisitiza Dkt. Nchemba.
Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alionyesha kuwa utekelezaji wa miradi ya masoko na miundombinu ya usafiri ni sehemu ya maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza ajira na kuinua uchumi wa wananchi katika maeneo ya mijini na vijijini.
“Maelekezo haya tunayoyatekeleza ni sehemu ya dhamira ya Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata mazingira bora ya kufanya kazi na kujipatia kipato,” alisema Waziri Mkuu.
Kuhusu Stendi ya Bunju, Waziri Mkuu alisema Serikali imepokea maoni ya wananchi kuhusu mpangilio wa usafiri na athari zake kwa gharama za maisha, hususan kwa abiria wanaolazimika kubadilisha magari zaidi ya moja. Ameelekeza mamlaka husika kufanya tathmini ya mpangilio huo ili kulinda maslahi ya wananchi bila kuathiri utoaji wa huduma za usafiri.
Aidha, katika hatua za awali za uendeshaji wa soko hilo, Waziri Mkuu ameagiza mamlaka husika zizingatie kupunguza au kuahirisha ushuru kwa kipindi maalum ili kutoa nafasi kwa wafanyabiashara kujiimarisha na kuvutia wateja. Amesema Serikali imejipanga kutenga fedha katika bajeti ijayo kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya masoko, ikiwemo barabara za kuingia sokoni, maeneo ya maegesho na mazingira rafiki yatakayochochea biashara na maendeleo ya maeneo yanayoyazunguka masoko hayo.
Akihitimisha ziara hiyo, Waziri Mkuu aliwataka wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kuwa makini na wageni wanaowapangisha nyumba zao, akibainisha kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakikodi nyumba kwa bei ndogo kisha kuzikodisha tena kwa bei kubwa, huku wengine wakizikodisha kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu vinavyohatarisha amani na usalama wa jamii.
“Wananchi wawe makini na wageni wanaowapangisha nyumba. Wengine wanazitumia vibaya nyumba hizo na kuhatarisha amani na usalama wa jamii,” alionya.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu aliambatana na viongozi wengine wakiwemo Waziri wa Maji, Jumaa Aweso; Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Jafar Seif; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, pamoja na viongozi wengine wa Serikali.




0 comments:
Post a Comment