Nafasi Ya Matangazo

December 15, 2023






Vijana wanaosimamia Itifaki kwenye dhifa mbalimbali za Kiserikali na hata za Taasisi binafsi wametakiwa kujitambulisha kwenye ofisi zao ili waweze kutambulika na kutumika kwa ajili ya kusimamia taratibu na ustaarabu wakati wa shughuli tofauti tofauti zinazotekelezwa Mkoa wa Dodoma na Mikoa mingine pia pindi huduma yao inapohitajika.

Hayo yameelezwa Leo Desemba 15, 2023 na Mhe. Rosemary Senyamule wakati akifungua mafunzo siku tatu yanayotolewa kwa timu ya huduma ya Itifaki yanayofanyika kwenye ukumbi wa Chuo kikuu cha Mipango kilichopo Jijini Dodoma.

"Nimetiwa Moyo na vijana hawa kwa kuweza kuhudhuria mafunzo haya. Dodoma ikiwa ndio makao makuu ya nchi, Kuna takribani ofisi 100 za Serikali hapa hali inayopelekea kuwa na matukio mengi yenye uhitaji wa huduma hii. Kumekua na changamoto kwenye suala la usimamizi wa Itifaki kwenye dhifa mbalimbali.

"Mafunzo haya yatawasaidia huko muendapo na nitoe Wito kwenu, baada ya mafunzo haya, mukajitambulishe kwenye ofisi zenu ili mukihitajika muweze kutumika. Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anahimiza kufanyika mikutano mbalimbali hali inayopelekea kuhitajika watu wenye sifa kama zenu. Mafunzo yenu yatakua na faida kubwa kwa Dodoma" Amesema Mhe. Senyamule.

Awali akitoa hotuba fupi ya Timu hii, Mwenyekiti wake Bw. Hussein Aboubakar Hussein, amesema vijana hawa wanashauku kubwa ya kufanya maendeleo kwenye sekta ya kilimo hivyo ametoa ombi kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa kupatiwa shamba la Hekari 50 na Mhe. Senyamule ameridhia ombi hilo na kuahidi kuwapatia kwa kuzingatia Mradi mkubwa wa Serikali wa BBT ulioanzishwa na Wizara ya Kilimo unaolenga vijana kujikita kwenye uwekezaji wa kilimo.

Pia timu hii imepata mafanikio kadhaa ikiwemo kutambulika na Mamlaka mbalimbali, kusimamia na kushiriki Itifaki wakati wa mbio za Mwenge, kupata usajili wa Kiserikali pamoja na kuandaa mradi wa kuwezesha watoto kwenda shule inayotarajiwa kuwa msaada kwa watoto ambao wanahitaji kwenda shule lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Timu ya Itifaki imesajiliwa tarehe 13 Machi 2023 kwa lengo kuu la kutoa huduma za kiitifaki na uendeshaji wa mikutano na dhifa mbalimbali ina washiriki 81 wakiwemo Maafisa Itifaki kutoka sehemu mbalimbali, waajiriwa na wasio waajiriwa kutoka Mikoa tofauti tofauti nchini.
Posted by MROKI On Friday, December 15, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo