Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule leo Disemba 8, 2023, amezindua gari mbili za Hospitali ya Taifa ya Afya ya akili Mirembe iliyopo katika Kata ya Hazina Jijini Dodoma ambapo kwa kipindi kirefu Hospitali hiyo imekua ikikabiliwa na ukosefu wa vitendea kazi hivyo.
Akizindua gari hizo ambazo moja ni kwa ajili ya kubebea wagonjwa na nyingine ni kwa matumizi ya kazi za kawaida za Hospitali, Mhe. Senyamule amesisitiza utunzaji wake.
"Serikali ya awamu ya Sita wakati huu imekua na kasi kubwa ya kuimarisha huduma za afya na kwa Mkoa wetu wa Dodoma kila ngazi imeimarika kwa nafasi yake. Kwa mwaka huu pekee kumekua na uzinduzi wa gari za wagonjwa ambapo Mkoa wetu umepata jumla ya gari 30 ambapo 10 ni kwa ajili ya kazi na 20 kwa ajili ya kubeba wagonjwa.
"Natoa shime kwa watumiaji wa gari hizi kuzitumia kwa utaratibu na miongozo ili ziweze kudumu kama ilivyotarajiwa hivyo vitendea kazi hivi vitumike vizuri. Afya ya akili ni tatizo linalohitaji kushughulikiwa mapema ili lisikufikishe sehemu mbaya. Huduma munayoitoa ikifikia watu wengi, itatengeneza utashi zaidi." Amesema Mhe. Senyamule.
Hata hivyo, Mkurungenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mirembe Dr. Paul Lawala, ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuleta vitendea kazi kwenye Hospitali yake kwani hapo awali walikua wakipata changamoto kwenye utekelezaji wa huduma hasa linapohitajika suala la usafiri kwani kwa Sasa wamepanua huduma za Hospitali za dharura na mahututi hivyo ujio wa gari hizi umefika wakati muafaka kutatua changamoto hiyo.
0 comments:
Post a Comment