CPA. Hosea Kashimba, Mkurugenzi Mkuu PSSSF
Na K-VIS BLOG/Khalfan Said, ARUSHA
MFUKO
wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umetenga muda maalum wa
majuma manne kuanzia Novemba 27 hadi Disemba 22, 2023, kwa lengo la kusikiliza
na kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za wanachama, Mkurugenzi Mkuu wa
Mfuko huo, CPA. Hosea Kashimba, amesema.
CPA.
Kashimba amesema hayo kwenye banda la PSSSF katika Maadhimisho ya Wiki ya
Huduma za Fedha Kitaifa, kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha
Novemba 24, 2023.
“Iwapo
kuna mwanachama yeyote mwenye changamoto yoyote inayohusu uanachama, michango
na mafao, afike katika ofisi za PSSSF zilizo jirani naye Tanzania bara na
Zanzibar, tutamsikiliza na kutatua changamoto yake.” Alisisitiza.
Alisema
zoezi hilo litakuwa likifanyika kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja
jioni, Jumatatu hadi Ijumaa.
“Lakini
hata baada ya kipindi hicho maalum kufikia ukomo, bado tutaendelea kuwapatia
huduma wanachama wetu, lengo hasa ni kuhakikisha wanachama wetu wanafurahia
huduma zetu wakati wote.” Alisema CPA. Kashimba.
Pia
amerejelea angalizo kwa wanachama na wastaafu, kuwa wasikubali kupokea
maelekezo yoyote kutoka kwa watu wasiowajua endapo wanahisi wanachangamoto
yoyote kuhusiana na uanachama wao au mafao yao.
“Tunawaasa
wanachama wetu hususan wale wanaokaribia kustaafu, watambue kuwa huduma zetu
zinatolewa bure bila malipo yoyote, na kama wanachangamoto yoyote wapige simu
namba ya bure 0800 110 040 au kupitia mitandao yetu ya kijamii kupitia anuani
ya PSSSFTZ.” Alifafanua CPA. Kashimba.
0 comments:
Post a Comment