Timu ya Mpira wa Miguu ya Tume ya Madini imetinga Robo Fainali Kibabe baada ya kuichakaza timu ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
kwa goli mbili kwa Moja
Katika mchezo huo uliochezwa leo Oktoba 07, 2023 katika uwanja wa Samora Mkoani Iringa, Timu ya Maendeleo ya Jamii ilikuwa ya kwanza kupata goli katika dakika ya 20 ya mchezo na mpaka timu zinaenda mapunziko, timu ya Maendeleo ya Jamii ilikuwa inaongoza kwa goli moja.
Katika kipindi cha pili timu ya Tume ya Madini ilianza kwa kasi sana kwa kulishambulia lango la Maendeleo ya Jamii na dakika ya 12 Kiungo Mshambuliaji wa Tume ya Madini, Frank Nagabona aliipatia Tume ya madini goli la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti.
Timu ya Tume ya Madini iliendelea kutandaza kandanda safi kwa kumiliki mpira na kulishambulia lango la Maendeleo ya Jamii ambapo katika dakika ya 23 ya kipindi cha pili, Tume ya Madini ilipata goli la Pili kupitia kwa Kiungo Mshambuliaji anayecheza namba 10 Waziri Nkuppe aliyepiga shuti kali nje na kumshinda mlinda mlango wa Maendeleo ya Jamii.
Mpaka mpira unamalizika, Tume ya Madini ilikuwa inaongoza kwa goli mbili kwa moja, ambapo matokeo hayo yamepelekea Tume ya Madini kutinga kibabe Robo Fainali ya Mashindano hayo.
Mara baada ya mchezo huo kumalizika, Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo ya Tume ya Madini ambaye pia Mshambuliaji wa Timu ya Tume ya Madini, Azihar Kashakara amesema kuwa ushindi huo unatokana na nidhamu ya wachezaji na mazoezi wanayofanya kila siku sambamba na ushirikiano na msaada mkubwa wanaopata kutoka kwa Viongozi wa Tume ya Madini,
Ameongeza kuwa, kupitia mashindano hayo wataendelea kuitumia fursa hiyo kuitangaza Tume ya Madini pamoja na majukumu yake, fursa mbalimbali zilizopo katika Sekta ya Madini na Dira ya Wizara ya Madini 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri.
Wakati huo huo wakizungumza kwa nyakati tofauti, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Eng. Yahya Samamba na Mkurugenzi wa Huduma za Tume, CPA William Mtinya wameipongeza timu ya mpira wa miguu na kuwataka washiriki wote wa Tume ya Madini kwenye mashindano ya SHIMIWI kuimarisha nidhamu na kutangaza Sekta ya Madini.










0 comments:
Post a Comment