Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia wakati wa ufunguzi wa
mkutano wa nane wa Majaji Wanawake ulioandaliwa na Chama Cha Majaji Wanawake
Tanzania (TAWJA) unaofanyika kila baada ya miaka miwili na mkutano wa mwaka huu
ulikuwa na kauli mbiu isemayo Kuongoza njia kufikia hitajio la upatikanaji wa
haki kwa wote na kwa wakati.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akihutubia wakati wa mkutano wa nane wa chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania uliofanyika kwenye ukumbi wa PSPF Golden Jubilee jijini Dar es Salaam.
Mhe. Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar,Mhe. Othman Makungu,akitoa nasaha zake wakati wa uzinduzi wa mkutano wa nane wa chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA)
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania Jaji Imani Aboud akitoa salaam za ufunguzi wa mkutano wa nane wa chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA)
Sehemu ya waliohudhuria wakiwa makini katika kuchukua yale yaliosemwa na Mhe. Makamu wa Rais wakati wa uzinduzi wa mkutano wa nane wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA)
***************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaagiza Majaji na Mahakimu wanawake kote
nchini kupambana ipasavyo katika kukabiliana vitendo vya rushwa,unyanyasaji
kijinsia na rushwa ya ngono ili kusaidia wanawake kupata haki zao za msingi
bila kubaguliwa katika jamii.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan
ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam wakati anafungua Mkutano Mkuu wa NANE wa
Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA).
Makamu wa Rais pia ameonya kuhusu
vitendo vya rushwa ya ngono inayofanywa na baadhi ya watendaji wenye madaraka
na kusema tabia hiyo ni mbaya na lazima ikomeshwa mara moja katika jamii.
Amesema kuwa vitendo hivyo vya rushwa
ya ngono huzuia na kukwamisha juhudi za wanawake kufikia huduma za kijamii na za
kiserikali ipasavyo ikiwemo elimu, ajira na haki kwa ajili ya ustawi wa
wanawake.
Aidha Makamu wa Rais Samia Suluhu
Hassan amekishukuru Chama cha Dunia cha Majaji Wanawake (IAWJ) kwa mchango na msaada
wake kwa TAWJA katika programu ya miaka mitatu ya kupambana na matumizi mabaya
ya madaraka na rushwa ya ngono.
Makamu wa Rais pia ameipongeza Wizara ya
Katiba na Sheria, Shirika la UN Women na wadau wengine wa TAWJA kwa kuunga mkono
mapambano ya aina zote za ubaguzi na ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini.
Amesema elimu ya haki za Binadamu
iliyotolewa na Chama hicho imeleta badiliko kwa wengi kwa njia ya mafunzo na
machapisho na jitihada hivyo lazima ziongezwe ili huduma hiyo iweze kuwafikia
wananchi wengi zaidi kote nchini.
Amesisitiza wanachama wa Chama cha TAWJA
waendelee kutoa msaada katika kuwasaidia wanawake na watoto ambao wanakandamizwa
kwa kunyimwa haki zao katika jamii ili waweze kupata haki zao nchini.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mohamed Chande Othman amemhakikishia Makamu wa Rais
kuwa mkakati wa uimarishaji wa shughuli za mahakama nchini unaendelea vyema lengo
likiwa ni kutenda haki kwa wananchi kote nchini bila ubaguzi.
Kauli mbiu ya Mkutano Mkuu wa NANE
wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TAWJA) “Kuongoza njia kufikia
hitajio la upatikanaji wa haki kwa wote na kwa wakati”.
No comments:
Post a Comment