January 06, 2017

MAKAMU WA RAIS AFANIKIWA KUINGIZA TANZANIA KATIKA MPANGO WA BIASHARA WA CHINA WA ONE BELT ONE ROAD

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wenyeviti wa TPSF,CTi,TCCIA na ZNCCIA juu ya mpango wa kibiashara unaojulikana kama China One Belt, One Road ulio asisiwa na serikali ya China na unajumuisha bara la Asia, Mashariki ya Kati,Ulaya na Afrika, Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Wenyeviti wa TPSF,CTi,TCCIA na ZNCCIA juu ya mpango wa kibiashara unaojulikana kama China One Belt, One Road ulio asisiwa na serikali ya China na unajumuisha bara la Asia, Mashariki ya Kati,Ulaya na Afrika.
 **************
Jitihada za Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan za kuiingiza Tanzania katika mpango mkubwa wa Biashara kwenye bara la Asia, Mashariki ya kati,Ulaya na Afrika  umefanikiwa baada ya Tanzania kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi Saba kuingizwa katika mpango unaojulikana kama China One Belt, One Road Stratergy.

Nchi nyingine ambazo zimechanguliwa kuingizwa kwenye mpango huo ni Malaysia,Sri lanka, Nepal, Bangladesh,Pakistan na Thailand.
Baada ya Tanzania kuingizwa rasmi katika mpango huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye pia Mjumbe katika jopo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la kumuwezesha mwanamke kiuchumi akiwakilisha nchi za ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika amekutana na Watendaji kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF),Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Biashara (TCCIA) na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) kuwaeleza kuhusu muhimu wa Tanzania kuingizwa kwenye mpango huo.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imepata uanachama wa mpango huo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mfanyabiashara wa Madini na Vito kutoka China Dkt Helen Lau kuhusu manufaa ya mpango huo na Makamu wa Rais alimwomba Mfanyabiashara huyo kuisaidia Tanzania kuingia kwenye mpango huo China One Belt, One Road Stratergy jambo ambalo limefanikiwa.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa Mwezi Septemba mwaka 2016 ulifanyika mkutano Guangdong nchini China kujadili maombi ya kujiunga na mpango huo ambapo Makamu wa Rais alimwomba Dkt Helen kuiwakilisha Tanzania katika kuwasilisha maombi na kwa bahati nzuri ombi la Tanzania lilikubaliwa na kupata uanachama katika mpango huo mkubwa wa China One Belt, One Road.

Makamu wa Rais amesema kuwa moja ya fursa zinazotolewa na Serikali ya China katika mpango huo ni kila nchi Mwanachama kupewa vyumba vya ofisi katika jengo linaloitwa 21st Century Maritime Silk Road Expo bila kulipa kodi ya pango kwa miaka Mitatu na baadhi ya vyumba vya jengo hilo vitatumiwa na nchi husika kuonyesha na kutangaza bidhaa zao.
Kufutia Tanzania kuingizwa kwenye mpango, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza watendaji wa sekta binafsi alikutana nao ikulu jijini Dar es Salaam wajipange na kuweka mikakati ya namna ya kunufaika na mpango huo haraka iwezekanavyo.

Amesisitiza kuwa mpango huo wa China One Belt, One Road Stratergy uliobuniwa na serikali ya China kwa dhamira ya kuzikutanisha Jumuiya za Wafanyabiashara za  Mashariki mwa bara Asia, Mashariki ya kati, Ulaya na Afrika kwa ajili ya kubadilishana mawazo,kuonesha njia na kupeana ushauri wa jinsi ya kukuza biashara kati ya nchi wanachama wa mpango huo kwa lengo la kuiwezesha sekta ya biashara kuchangia nyema kwenye uchumi wa mataifa yao.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania baada ya kuingia kwenye mpango huo itanufaika na fedha za mfuko kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu ambazo zinatolewa kwa nchi zilizojiunga na mpango huo.

Kwa upande wake, Mweyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania Godfrey Simbeye na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar Taufik Turki wamemuahidi Makamu wa Rais kuwa watatumia fursa hiyo ipasavyo ili kukuza biashara kati ya Tanzaniana Nchi wanachama wa mpango huo.

No comments:

Post a Comment