December 01, 2016

Kampuni ya Puma Energy Tanzania yajivunia kuutangaza Utalii wa Tanzania

Wafanyakazi wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania, Mwenyekiti wa Bodi, Mkurugenzi wa Masoko wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya marubani wa ndege za kizamani mara baada ya kuwasili Zanzibar.
Meneja Mkuu wa kampuni ya Puma Energy  Tanzania, Philippe Corsaletti akizungumza  katika hafla maalum baada ya kuwasili  jumla ya ndege 22 za kizamani  zilizotengenezwa kati ya miaka 1920 na  1930 kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar jana.
 Mwenyekiti wa bodi ya Puma Energy  Tanzania,  Dk Ben Moshi (wapili kushoto)  akisalimiana na rubani pekee wa kike  katika mashindano ya kurusha ndege za  kizamani zilizotengenezwa kati ya mwaka  1920 na 1930 mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid  Amani Karume, Zanzibar, wa kwanza kushoto  ni Mkurugenzi wa Masoko wa Kamisheni ya  Utalii Zanzibar, Dk Miraj Ussi na wa pili  kulia ni Meneja Mkuu wa Puma Energy  Tanzania, Dk Ben Moshi.
Moja ya ndege ya kizamani iliyotengenezwa  kati ya miaka 1920 na 1930 ikiwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume katika moja ya mashindano ya ndege hizo yajulikanayo kwa jina la "Vintage Air Rally" yaliydhaminiwa na Kampuni ya Puma Energy  Tanzania.
Mkurugenzi wa Masoko wa Kamisheni ya  Utalii ya Zanzibar, Dk Miraj Ussi  akizungumza katika hafla ya kuzipokea  jumla ya ndege 22 za kizamani  ziliyotengenezwa kati ya miaka 1920 na  1930 mara baada ya kuwasili kwenye uwanja  wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume katika moja ya mashindano ya ndege  hizo yajulikanayo kwa jina la "Vintage Air  Craft Rally"
 Baadhi ya ndege za kizamani  zilizotengenezwa kati ya miaka 1920 na
1930 zikiwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar jana.
Mkurugenzi wa Vintage Rally, Sam Rutherford akizungumza mara baada ya kuwasili kwa ndege za kizamani zilizotengenezwa kati ya miaka 1920 na 1930 zikiwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar jana. Rutherford aliipongeza kampuni ya Puma Energy kwa kufanikisha mashindano  hayo
***************

Na Mwandishi wetu 
Kampuni ya Puma Energy Tanzania imesema itaendeleza jukumu la kuutangaza Utalii wa ndani ya Tanzania nje ya mipaka yake ili kuwawezesha wataalii wengi kuja nchini na kuongeza pato la taifa. 

Kauli hiyo imetolewa na Meneja Mkuu wa kampuni ya Puma Energy Tanzania, Philippe Corsaletti mara baada ya kuwasili jumla ya ndege 22 za kizamani zilizotengenezwa kati ya miaka 1920 na 1930 kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar jana. 

Corsaletti alisema kuwa jukumu la kuutangaza utalii wa Tanzania halipo kwa serikali pekee, kwani hata wadau wanafursa ya kufanya hivyo ili kuendelea kuleta tija nchini. 

Alisema kuwa jumla ya marubani 48 kutoka ndege 22 wameshiriki katika mashindano ya ndege za zamani maarufu kwa jina la “ Vintage Air Rally” yenye lengo la kuutangaza utalii nchini na ushiriki wao mbali ya kujitangaza, pia ni sehemu ya kushiriki katika kazi za kijamii kwani mashindano hayo pia yanachangisha fedha kwa ajili ya shughuli za Unicef, Bird Life International na Seed Bombing. 

“Mbali ya marubani na waongoza ndege, pia kuna washiriki wengine ambao wameambatana na ndege hizi kwa ajili ya kazi mbalimbali, hao wote watashindana katika hifadhi na kuona vivutio vya utalii na kwenda kuvitangaza nje ya nchi, hii ni fursa pekee ya kuvitambulisha duniani,” 

“Kampuni ya Puma Energy Tanzania imeshiriki ipasavyo kuhakikisha ndege zote zinapata mafuta ya kutosha aina ya Avigas mbayo kampuni yetu pekee ndiyo inazalisha mafuta haya ambayo ni ya ubora wa hali ya juu, mbali ya kupita katika mbuga ya Ngorongoro na kujionea utititiri wa wanyama na vivutio mbalimbali, baada ya hapo watapita Dodoma, Songwe (Mbeya) kabla ya kuelekea Zambia,” alisema Corsaletti. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi ya Puma Energy Tanzania, Dk Ben Moshi aliipongeza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kukubali ndege hizo kutua na kupata huduma ya mafuta huku maribani wake wakijionea vivutio mbalimbali vya utalii. 

“Tumefarijika na ushirikiano tulioupata kutoka viongozi na kuwezesha tukio hili la kihistoria kufanyika kwenye uwanja wa ndege na watu mbalimbali kujionea ndege hizi za kizamani lakini bado zinauwezo wa kuruka umbali mrefu, kampuni yetu imefurahia sana nahasa jukumu la kuwa wadhamini wa mashindano haya,” alisema Dk Moshi. 

Dk Moshi alisema kuwa mashindano hayo yamefungua ukurasa mpya kwa kampuni ya Puma Energy kwa upande wa biashara na hasa ubora wa bidhaa zake ambazo mpaka sasa zimewavutia na zinaendelea kuwavutia wateja wengi. 

Mkurugenzi wa Masoko wa Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar, Dk Miraj Ussi aliipongeza kampuni ya Puma Energy Tanzania kwa kuchagua Zanzibar kuwa moja ya kituo cha mashindano ya ndege hizo ambazo zenyewe ni kivutio pekee. 

Dk Ussi alisema kuwa mashindano hayo ya Ndege za zamani yataendelea kuutangaza utalii wa Zanzibar na kuwendelea kuwa maarufu zaidi na kuwafanya watalii wengi zaidi kutembelea kujionea utajiri mkubwa wa nchi. 

“Ni faraja kuwa miongozi mwa mashindano haya, kwa kweli yametuvitia sana kwani yataendelea kututangaza nje ya mipaka yetu, tuna vivutio vingi sana hapa, tunawaomba mashindano mengine yaanzie hapa,” alisema Dk Ussi. 

Mkurugenzi wa Vintage Rally, Sam Rutherford aliipongeza kampuni ya Puma Energy kwa kufanikisha mashindano hayo huku akivutiwa na vivutio mbalimbali vya utalii vya Tanzania. “Tumependa sana Zanzibar, tumeona vivutio kadhaa vya utalii, bado tutaendelea kuona, kwani mashindano yanaendelea,” alisema Rutherford. 

Vintage Air Rally inahusisha ndege za zamani za kati ya miaka ya 1920 na 1930 ambazo zinarushwa na marubani wenye uzoefu mkubwa kutoka sehemu mbalimbali duniani, wakiruka kukatisha Afrika kutoka katika visiwa vya Crete nchini Ugiriki hadi Cape Town Afrika ya Kusini. 

Shindano hili lilianza tarehe Novemba 12, Crete, Ugiriki na safari yote itachukua siku 35 wakipita katika jumla ya nchi 10 ambazo ni Ugiriki, Misri, Sudan, Ethiopia, Kenya, Tanzania na kuendelea Zambia, Zimbabwe, Botswana na Afrika ya Kusini.

No comments:

Post a Comment