Waziri
Mkuu,Kassim Majaliwa na Mkewe Mary (kushoto) wakipata maelezo kutoka
kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama kuhusu ujenzi wa makazi mapya ya
Waziri Mkuu, kwenye kilima cha Mlimwa mjini Dodoma Septemba 7, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary (kulia kwake ) wakikagua
ujenzi wa makazi mapya ya Waziri Mkuu kwenye kilima cha Mlimwa mjini
Dodoma Septemba 7, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Badhi ya Mawaziri na viongozi wa
mkoa wa Dodoma baada ya kukagua ujenzi wa makazi mapya ya Waziri Mkuu
kwenye kilima cha Mlimwa mjini Dodoma Septemba 7, 2016. Katikati ni
mkewe Mary.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). SOMA ZAIDI BOFYA HAPA
***************
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa
makazi mapya ya Waziri Mkuu katika eneo la Mlimwa na kuagiza umalizike
kwa wakati ili aweze kuhamia kama alivyoahidi.
Katika ziara hiyo
aliyoifanya leo mchana (Jumatano, Septemba 7, 2016) Waziri Mkuu amesema
ameridhishwa na namna kazi ya ujenzi inavyofanyika.
“Nimekuja kukagua
makazi mapya na mahali pa kufanyia kazi. Kazi ya ujenzi inaendelea vizuri, nimejionea
mwenyewe na naamini katika kipindi kifupi watakuwa wamekamilisha,” amesema.
Amesema kutokamilika
kwa ujenzi huo hauwezi kukwamisha azma yake ya kuhamia Dodoma kwa sababu tayari
inafahamika kuwa Makao Makuu ya Ofisi ya
Waziri Mkuu yako Dodoma.
Amesema uamuzi wa
Serikali kuhamia Dodoma hautokani na shinikizo la kisiasa bali ni utekelezaji
wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa
Oktoba Mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.
“Tangu wakati huo Serikali zote ziliendelea
kufanya juhudi mbalimbali za kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne
ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo,” amesema.
“Pia tukumbuke kauli
ya Mheshimiwa Rais aliyotoa kwenye hotuba yake ya Julai 23, 2016 alipochaguliwa
kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM, na akairudia tena Julai 25, kwenye maadhimisho ya
kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo hiyo nikaweka msisitizo,” amesema.
Amesema uamuzi wa
Serikali ya awamu ya tano wa kuhamia Dodoma unakuja baada ya kuridhishwa na ujenzi
wa miundombinu na maeneo ya kutolea huduma za kijamii kwa wageni na wenyeji
ikiwemo Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)
yenye uwezo wa kutibu magonjwa makubwa kama ya moyo na figo.
Waziri Mkuu amesema
tayari Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ina mpango kamambe (master
plan) na ina viwanja vya kutosha kujenga makazi na ofisi mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment