Inspekta Jenerali wa
Polisi IGP Ernest Mangu
INSPEKTA Jenerali wa
Polisi IGP Ernest Mangu anatarajia kukabidhiwa uenyekiti wa Shirikisho la wakuu
wa Majeshi ya Polisi kusini mwa Afrika (SARPCCO) katika mkutano unaotarajiwa
kufanyika tarehe 16 Septemba, 2016 jijini Arusha. IGP Mangu atakabidhiwa
uenyekiti huo kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi wa nchi ya Msumbiji ambapo
atadumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Mkutano huo utatanguliwa
na mkutano wa kamati tendaji za SARPCCO amabazo zitakutana Septemba 14 na 15
mwaka huu ili kuandaa ajenda na
mapendekezo ambayo yatawasilishwa katika
mkutano wa wakuu wa Polisi ambao unatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Katika mkutano huo mambo
mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu yatajadiliwa ikiwemo uhalifu wa kuvuka mipaka,
pamoja na kuweka mikakati na maazimio ya kufanya Oparesheni za pamoja zinazojumuisha
nchi zinazounda shirikisho hilo.
Vilevile, mkutano huo
utajadili kwa kina utekelezaji wa maazimio mbalimbali kupitia kamati tendaji za
wakurugenzi wa upelelezi, kamati tendaji
ya sheria, kamati tendaji ya mafunzo na kamati tendaji ya mtandao wa Polisi
wanawake.
Aidha, suala la michezo
baina ya Majeshi ya Polisi kwa nchi wanachama nalo litajadiliwa katika mkutano
huo.
SARPCCO iliundwa mwaka
1995 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za
kusini mwa Afrika katika kukabiliana na uhalifu. Mpaka hivi sasa umoja huo
unaundwa na Nchi kumi na tano ambazo ni Tanzania, Angola, Botswana, Malawi,
Lesoto, Mauritius, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), Msumbiji, Namibia,
Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Swaziland, Madagascar na Seychelles.
0 comments:
Post a Comment