September 07, 2016

DAWASCO YAANZA KUONDOA MITA CHAKAVU KWA WATEJA WAKE



Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Cyprian Luhemeja.
 SHIRIKA la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) limeanza zoezi la kuondoa mita za maji zote chakavu katika jiji la Dar es salaam ili kupunguza tatizo la upotevu wa maji linaloendelea kuikumba shirika hilo.

Hayo yameelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Cyprian Luhemeja wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

“Tayari Dawasco ina mpango wakubadilisha mita za Maji zote zenye umri mkubwa kwenye maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na maeneo ya mkoa wa Pwani ila tutaanzia na maeneo ya Magomeni, Kawe pamoja na Kinondoni kwa kuwa mita nyingi za maji huko zina umri wa zaidi ya miaka 10 hivyo tayari mita laki moja zimeshaagizwa kwaajili zoezi hilo, “alisema Luhemeja.

Aliongeza kuwa jumla ya mita 100,000 tayari zimeshaagizwa kwa ajili ya zoezi hilo huku akibainisha kuwa maeneo ya Kawe, Kinondoni pamoja na Magomeni ndiyo yatakayoanza zoezi hilo.

Aidha amewataka wateja wenye matatizo na mita zao za maji kutumia zoezi hilo kubadilisha mita zao ili kupunguza malalamiko ya upotevu wa maji na uchakavu wa mita zenyewe.

Luhemeja ametoa wito kwa wateja wote kuhakikisha kuwa mita zote za maji zinawe kwa nje ya uzio wa nyumba ilikuwezesha maafisa wa Dawasco kuzifuatilia na kusoma matunzi yake ya kila mwezi na kuzifanyia marekebisho kila zipatapo  matatizo ikiwemo ya uvujaji pia amesema mita za maji zikiwa ndani ya uzio huleta mwanya kwa baadhi ya wananchi kufanya wizi wa maji kwa kuzichezea mita hizo.

“Mita zote za maji zinatakiwa ziwe nje ya uzio wa nyumba ilikuwezesha maafisa wa Dawasco wanaopita kila mwezi kusoma matumizi ya maji ya kila mwezi wawezi kusoma na pia kupata taarifa za mita pale inapokuwa na hitilafu kama uvujaji iweze kurekebishwa nakufanyiwa kazi kwa wakati, “alisema Luhemeja.

Hata hivyo mhandisi Luhemeja amewasihi wananchi wote ambao wanamatatizo mbalimbali ya uvujaji wa mita au kupata ankara za maji kubwa zisizoakisi matumizi yao kutokana ubovu wa mita wasisite kufika kwenye ofisi za Dawasco kwa ajili kutoa taarifa itakayowezesha tatizo husika kushughulikiwa kwa wakati.

No comments:

Post a Comment