Rais Dk John Pombe Magufuli akiwa na Mke wake Mama Janeth
Magufuli wakisali katika ibada ya Jumapili katika Kanisa la Bikira Maria
Parokia ya Chato mkoani Geita.
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akisalimiana na na Padre wa
Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato Henry Mulinganisa mara baada ya
kuwasili kwenye kanisa hilo.
Rais Dk John Pombe
Magufuli akiimba wimbo wa Amani pamoja na Kwaya ya Kanisa la African Inland Church la Chato Mkoani Geita
mara baada ya kuwasili katika kanisa hilo.
Shekhe
wa Bakwata Wilaya ya Chato Hassan Issa Mnubi akiongoza dua ya Kumuombea Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Mkewe Mama
Janeth Magufuli nje ya Msikiti wa Omar Bin-L-Khattab Chato Mkoani Geita. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI
***********
RAIS Dkt. John
Pombe Magufuli leo tarehe 07 Agosti, 2016 ametembelea Msikiti na Makanisa yaliyopo
Chato Mjini Mkoani Geita na kuendelea kuwasihi Watanzania kuombea amani na
utulivu katika nchi bila kujali tofauti za dini, makabila na kanda wanazotoka.
Rais Magufuli
ametoa ujumbe huo mara baada ya kusali ibada ya Jumapili katika Kanisa Katoliki
la Bikira Maria Parokia ya Chato, na baadaye kutembelea Kanisa la Anglikana la
Mtakatifu Stephano Parokia ya Chato, Kanisa la African Inland Church la Chato
na kumalizia katika Msikiti wa Omar Bin -L-Khattab wa Chato.
Dkt. Magufuli
amesema pamoja na Watanzania wote kuungana kuombea amani na utulivu pia hawana
budi kutekeleza kwa vitendo Maandiko Matakatifu ya Biblia yasemayo
"Asiyefanya kazi na asile" kwa kuhakikisha kila mmoja anachapakazi
kwa juhudi na maarifa ili kuharakisha maendeleo ya Taifa.
"Ndugu zangu
nawashukuru sana, muendelee kuliombea taifa hili, taifa letu ni la umoja, sisi
wote ni Watanzania, tuendelee kumuomba mola wetu, kudumisha amani yetu, kujenga
umoja wetu kwa dini zote, makabila yote na vyama vyote, kwa sababu mola wetu
anatupenda sisi sote" Amesema Rais Magufuli.
Aidha, mara baada
ya kuwasalimu waumini wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Parokia ya Chato, Rais
Magufuli ameendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo jipya la Kanisa hilo
ambapo amefanikiwa kukusanya Shilingi Milioni moja za papo kwa papo.
Tayari Dkt.
Magufuli alishachangia ujenzi huo kwa kutoa Shilingi Milioni kumi tarehe 03 Aprili,
2016 na ametoa wito kwa watu mbalimbali kujitokeza kuchangia ujenzi wa Kanisa hilo.
Katika Msikiti wa
Omar Bin-L-Khattab na Makanisa ya Anglikana na African Inland Church Rais
Magufuli amechangia Shilingi Milioni tano kwa kila moja kwa ajili kuendeleza na
kukarabati majengo.
No comments:
Post a Comment