Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli (pichani) amewaagiza viongozi wote wa
kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Kitongoji hapa nchini kufuatilia matumizi ya fedha
zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo kwa lengo la
kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya fedha hizo.
Rais Magufuli
ametoa maagizo hayo leo tarehe 01 Agosti, 2016 katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika uwanja wa Mnadani na kuwajumuisha wananchi wa Katoro na
Buseresere Mkoani Geita.
Katika agizo hilo
Dkt. Magufuli amewaonya walimu ambao wameanza kufanya udanganyifu kwa
kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi kuliko idadi halisi kwa lengo la kupata
mgao mkubwa wa fedha za ruzuku na amesema Serikali itachukua hatua kali dhidi
ya yeyote atakayebainika kufanya hivyo.
"Ninafahamu
mgao wa fedha hizo hutolewa kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo, wapo
baadhi ya walimu ambao wameanza kuandika wanafunzi hewa katika shule zao, ili
kusudi aletewe hela nyingi kuliko idadi ya wanafunzi waliopo, wanafunzi kama
wapo laki nne yeye anasema shule yangu hii ina wanafunzi laki tano, ili kusudi
hela zikija za wanafunzi laki tano, za wanafunzi laki moja wagawane.
"Napenda
nitoe wito kwa walimu Tanzania nzima, mnatafuta matatizo, narudia mnatafuta matatizo,
msijaribu kula hela ya Serikali" Amesema
Rais Magufuli.
Pamoja na agizo
hilo, Rais Magufuli pia ametaka viongozi wa ngazi zote katika Mikoa kuhakikisha
wana takwimu za idadi ya wanafunzi katika shule zote zilizopo katika maeneo yao
ili kurahisisha ufuatiliaji wa fedha hizo na amesema kuwa kuanzia sasa ataanza
kutembelea shule kwa kushitukiza na kwamba kiongozi atakayeonekana kutojua
takwimu itakuwa ni uthibitisho kuwa hatoshi kuendelea na wadhifa alionao.
"Na nitoe
wito kwa viongozi wa Mikoa, Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi,
Makatibu Tarafa, Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji, kila mmoja awe na
idadi ya wanafunzi waliopo katika shule zao, hatutaki kuwapunja wanafunzi hela
ambayo wanatakiwa kupata, lakini pia hatutaki kutoa hela ambayo haitakiwi"
Amesisitiza Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli
ambaye ametumia mkutano huo kueleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali
yake ya Awamu ya Tano, kutekeleza ahadi yake ya kujenga Tanzania Mpya pia
amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa
kutembelea wananchi wanaowaongoza badala ya kukaa muda mwingi ofisini huku
akisisitiza ofisi hizo kuwepo katika maeneo yenye shughuli husika.
Aidha, Dkt.
Magufuli amekosoa utaratibu unaotumiwa na Halmashauri nyingi za Majiji,
Manispaa, Miji na Wilaya kutumia mawakala katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri
akisema mawakala hao wamekuwa wakitumia utaratibu huo kukusanya fedha nyingi na
kisha kuwasilisha kiasi kidogo katika Halmashauri husika.
"Hivi kwa
nini Halmashauri msingekuwa na maafisa wenu wazuri na mkawa na mashine za
kielektroni kwa ajili ya kukusanya fedha? Amehoji
Dkt. Magufuli na kuongeza kuwa "tena mawakala wengine ndio hao hao wamekuwa
wakikusanya kodi hata kwa wananchi wanyonge wenye vibiashara vidogo vya kuuza
mchicha bila hata kuwaonea huruma"
Rais Magufuli
ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amemaliza ziara yake ya siku
nne katika Mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita na yupo nyumbani kwake
Chato Mkoani Geita kwa mapumziko mafupi.
0 comments:
Post a Comment