Kwangu Kulwa akiwa kazini katika kiwanda cha TBL Mwanza
Mariam Zayumba akiwa kazini katika kiwanda cha TBL Mwanza.
**************
KAMPUNI ya TBL Group imeeleza kuwa itaendelea kuwaunga mkono vijana wa
kitanzania kwa kuwawezesha kupata elimu ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA
kupitia mpango maalumu wa kupata elimu zaidi ya vitendo kuliko nadharia unaojulikana
kitaalamu kama Dual Apprenticeship programme
Mpango huu unaoendeshwa na serikali kupitia taasisi zake za
mafunzo ya ufundi kwa kushirikiana na Chama cha Wenye Ujuzi cha Hamburg,
Ujerumani umelenga kuwapatia vijana mafunzo ya vitendo ambapo wanasoma wakiwa
wanapatiwa mafunzo ya vitendo kwenye viwanda na taasisi mbalimbali.
Meneja wa Mafunzo wa TBL Group ,Gasper Tesha amesema kuwa mpango huu
ulioanzishwa miaka 3 iliyopita umeonyesha maendeleo mazuri na makubwa ikiwa ni
pamoja na kuwanufaisha vijana hao kiutendaji kazi katika sehemu mbalimbali
kutokana na ujuzi waliopatiwa. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
Alisema vijana 4 waliofadhiliwa na kampuni hiyo na kupatiwa mafunzo
katika fani ya umeme wa viwandani wameweza kupata maarifa makubwa ya kazi kwa
vitendo kwenye kiwanda cha TBL cha Ilala ambapo baada ya kuhitimu masomo
wameweza kuajiriwa na wanaendelea kufanya vizuri.
Tesha alisema kampuni itaendelea kuunga mkono jitihada za serikali za
kuwawezesha watanzania wengi kupata ajira na kuwa na maisha bora na ndio maana
imeweza kutoa maelfu ya ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja
kupitia uwekezaji wake hapa nchini.
“Tutaendelea kuwafadhili vijana na kushiriki kuwapatia mafunzo ya
vitendo kupitia mpango huu kama ambavyo tumekuwa tukifanya kazi na makundi
mbalimbali na kuyapatia ujuzi na kuyawezesha kujiajiri mfano wakulima wa
Shahiri na zabibu tunaoshirikiana nao katika utekelezaji wa mpango wetu wa Go
Farming”Alisema.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo haya ambao wamefadhiliwa na TBL
Group na kupata ajira za kudumu baada ya mafunzo wamesema mpango huu ni mzuri
na wa aina yake ambao ukiungwa mkono utawezesha Tanzania kuwa na mafundi wazuri
wenye ujuzi mkubwa.
Mariam Zayumba ambaye anafanya kazi katika kiwanda cha TBL cha Mwanza
alisema kuwa hivi sasa yeye ni fundi mzuri wa umeme wa majumbani na
viwandani na anashukuru kupata mafunzo ya vitendo kwenye kampuni ambayo
imemuajiri kwa hivi sasa ya TBL Group kwa kuwa inavyo vifaa vya kisasa vya
kujifunzia na wataalamu waliobobea katika fani yake ya umeme ambao
wamemfundisha na anajiamini kuwa ni fundi mzuri wa umeme.
Naye Kwangu Kulwa ambaye naye anafanyia kazi katika kiwanda
cha TBL cha Mwanza anasema kuwa mpango huu wa Dual Apprenticeship
Training unamwezesha mtu kupata ujuzi wa fani husika wakati anafanya kazi
kwenye kiwanda hivyo kumuwezesha kwa kiasi kikubwa kujifunza zaidi kwa vitendo
na kuendana na mahitaji ya soko la ajira pmaoja na kupata uzoefu na uelewa wa
mazingira halisi ya kufanyia kazi.
Alitoa wito kwa vijana wenzake kujitosa zaidi katika fani ya ufundi kwa
kuwa kwa kiasi kikubwa inawawezesha kujipatia fursa za kujiajiri badala ya
kukata tamaa na kushinda wanalalamika kuwa hakuna ajira. “Nashukuru kwa kupata
fursa ya kufanya kazi kwenye kampuni hii na nimeweza kujifunza mambo mengi
hususani utumiaji wa zana za kisasa katika fani ya umeme”.
0 comments:
Post a Comment