TUKIO la kupatwa kwa jua kipete ambalo linataraji kutokea mwezi Septemba mwaka huu nchini hasa Mkoani Mbeya katika Wilaya ya Mbarali Kata ya Rujewa ni tukio la kisayansi ambalo kama nchi italitumia vyema ni fursa pekee ya kuweza kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii. Mwandishi Mroki Mroki "Father Kidevu" anaadika zaidi juu ya tukio hilo na mahusiano yake katika utalii.
Mtaalam wa Astronomia (Astronomy) kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) Dk. Noorali Jiwaji wa Kitivo cha Sayansi, Teknologia na Elimu ya Mazingira, akionesha kifaa maalum cha kutazamia jua linapo patwa. Kulia ni Kaimu Mkuu wa chuo hicho kikuu Huria, Profesa Elifas Tozo Bisanda.
***********
KUPATWA kwa
jua kunatokea wakati mwezi unafunika jua.
Matokeo yake ni kupungua kwa jua hadi kutoonekana
tena na kufika kwa giza wakati wa mchana. Muda wa kufunikwa kabisa ni dakika
chache tu.
Kupatwa kwa jua kunatokea kama dunia, mwezi na jua
vyote kwa pamoja vitakaa kwenye mstari mmoja mnyoofu yaani wakati mwezi unapita
kati ya dunia na jua.
Katika hali hiyo kuna kivuli cha mwezi kwenye uso
wa dunia. Kivuli hiki hakifuniki dunia yote. Kwa hiyo kupatwa kwa jua
kunaonekana kwa watu wengi kama kupungua kwa mwanga wa jua.
Kisayansi kuna aina mbalimbali za kupatwa kwa jua.
Miongoni mwa aina hizo ni kupatwa kwa
jua kabisa; hii jua ninapotea kabisa
kwa dakika chache. Hali hii huonekana kwenye kanda nyembamba duniani kinapopita
kitovu cha kivuli.
Aina nyingine ya kupatwa kwa jua ni kupatwa kipete; hapa mwezi huonekana
mdogo kuliko jua. Hivyo duara la kung'aa kwa jua huonekana kubwa kuliko duara la
mwezi na mwanga wa jua waonekana kama pete.
Pia aina nyingine ni kupatwa kwa jua kisehemu; hapa ni kuwa eneo kubwa la kivuli cha
kando watu huona upungufu wa mwanga. Kiasi chake hutegemea umbali na kitovu cha
kivuli. Ukitazama jua kwa filta kwa mfano kioo kilichopakwa dohani katika moshi
wa mshumaa huwa wanaona sehemu ya duara ya jua imefunikwa.
Miongoni mwa aina hizo tatu za kupatwa kwa jua,
huenda msomaji ulisha wahi kuona aina hizi kutegemea na umri wako. Laiki kwa
kizazi cha sasa sina hakika sana kama wamewahi kuona aina hizo za kuaptwa na
jua.
Mwezi Septemba mwaka huu kunatarajiwa kutokea tukiko
kubwa la angani la kipekee la kupatwa kwa jua usawa wa Tanzania ambalo
litatokea Septemba 1, mwaka huu, kuanzia saa 4:17 asubuhi hadi Saa 7:56
adhuhuri.
Washabiki na wanataaluma wa anga kutoka duniani
kote pamoja na wanasansi, wanafunzi pamoja na jamii ya watanzania wataelekea Wilayani
Mbarali katika Kata ya Rujewa, mkoani Mbeya kushuhudia duara la jua
linavyobadilika kuwa pete ya jua.
Ugeni huo mbali na kuwa wanakuja katika tukio la kisayansi lakini pia, ni fursa pekee katika sekta ya utalii kwani wageni wengi watakao kuja nchini wanahitaji kushawishwa kuweza kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini hasa vile vya mikoa ya Morogoro, Iringa na Mbeya. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI MAKALA HAYA
Katika tukio hili la kupatwa kwa jua, watu
wanaoishi ndani ya ukanda wenye upana wa kilomita 100 unaokatisha Kusini ya
Tanzania kutoka Congo kuelekea Katavi, mbeya, Ruvuma hadi Masasi na kuingia
Msumbuji, siku hiyo jua kama duara jembamba kama pete kwa vile asilimia 98 ya
jua litakuwa limejificha nyuma ya mwezi.
Tayari wa taalam wa elimu ya mambo ya anga ya Astronomia
(Astronomy) kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), wameaza mkakati wa
jinsi Chuo hicho kinavyoweza kwenda na wakati hasa katika mambo ya kisayansi na
kutoa elimu kwa wananchi juu ya tukio hilo kubwa la kihistoria litakalo tokea
nchini.
Kaimu Mkuu wa Chuo hicho cha OUT, Profesa Elifas
Tozo Bisanda amesema kuwa watatoa mafunzo hayo ya Sayansi katika kitivo chao
cha Sayansi ili kusaidia jamii kwenda na
teknolojia ikiwa ni pamoja na kutoa elimu hususani mashuleni ili jamiii itambue
juu ya tukio hilo la jua kupatwa kipete, kwa kutumia wataalam wa Chuo hicho.
Aidha watanzania wametakiwa kujiandaa kufuatilia
tukio hilo sambamba na kutengeneza fursa za kujiongezea fursa za kiuchumi
kutokana na ugeni mkubwa wa ndani na nje ya nchi utakaoshuhudia tukio hilo.
Inaelezwa kuwa, kwa mara ya mwisho kutokea kwa
tukio la kupatwa kwa jua lilionekana nchini Aprili 18, 1977 na kwamba litatokea
tena Mei 21, 2031.
Mhadhiri wa Fizikia, Kitivo cha Sayansi,
Teknolojia na Elimu ya Mazingira kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk
Noorali Jiwaji alisema tukio hilo litawafundisha wanafunzi kwa vitendo sayansi
ya astonomia na kuelewa namna jua na mwezi vinavyopangika angani.
Dkt. Jiwaji anasema, tayari wanaendelea na
taratibu zote ikiwemo suala la kutoa elimu katika eneo hilo la Rujewa Mkoani Mbeya hususani kwa wananchi
kuwa na tahadhari kuangalia jua hilo ikiwemo kutakiwa kutumia kitazama jua
ambacho ni kifaa maalum kitakachokuwa
kinachuja nguvu ya jua ambacho pia kinaondoa mionzi haribifu kwa asilimia
99.999.
“Kupatwa huko kwa jua kunaweza kuonekana kwa
usalama na watazamaji, lakini inabidi kutumia vichuja maalum vya mwanga wa
jua,” alieleza Dk Jiwaji.
Tukio la kupatwa ni la kusisimua na la nadra sana
kutokea katika maisha ya mtu. Hasa kwa kizazi hiki kipya ambacho kimechangamka
kitasisimuliwa sana na tukio la ajabu kama hili na watajifunza Sayansi ili
kuelewa kwa nini kinatokea kile wanachokiona.
Dk Jiwaji anaeleza kuwa tukio hilo linaweza
kutumiwa na shule na taasisi za elimu kuendeleza Sayansi na kuvuta wanafunzi
kujiendeleza kisayansi na hasa kuelewa mizunguko mbalimbali iliyopo katika
mfumo wetu wa sayansi pamoja na anga za juu kwa ujumla. Kuongeza uelewa wa
sayansi ni muhimu katika kuelewa maumbile ya ulimwengu wetu.
Kupatwa huku kutatokea siku ya Alhamisi ambapo
wanafunzi wengi watakuwa mashuleni na ni wakati wa masomo.
Kwavile mchakato wote utaendelea kwa Saa nne hivi , kati ya Saa 4 asubuhi hadi Saa 8
mchana wanafunzi wataweza kushirikiana
kuangalia na kusimulia na kujadili tukio ili kulielewa vizuri na
kuandika ripoti madarasani kwao.
Tukio jingine kubwa la kupatwa kwa jua kama hili
halitatokea jingine kwa miaka 15 ijayo, kwa hiyo tunahitaji kutumia fursa hili
kwa ukamilifu.
Mtaalaam huyo kutoka OUT, Dk Jiwaji anasema ili kuangalia
kupatwa huko, kila mmoja atahitaji kutumia kikinga macho kinachochuja mwanga wa
jua kiitwacho kitazamia jua. Nihatari
sana kuangalia jua kwa macho ya moja kwa moja au hata kutumia vichujio vingine
vya kiza vilivyotengenezwa kibinafsi.
Kitazamia jua maalum ni kifaa rahisi
kilichotengenezwa kutokana na kichuja nguvu ya jua ambacho kinaondoa mionzi
haribifu kwa asilimia 99.999. Miwani hiyo maalum ya jua inaweza kutengenezwa
Tanzania kwa gharama isiyozidi 500/= kila moja, ikiwemo kuchapa fremu za
kadbodi na kichuja nguvu ya jua (polymer filter) kinachoagizwa kutoka Marekani.
Aidha, alisema kuna madhara makubwa endapo
wananchi hawatahamasishwa kutoangalia jua kwa kutumia njia za asili ikiwemo
chupa na X-ray au negative za mikanda ya picha badala yake watumie kichuja
mwanga maalumu kilichotengenezwa kitaalam.
Utalii kutokana na kupatwa kwa jua kipete
Kupatwa kwa Jua kipete pia kuna weza kutumika kama
sehemu ya kuongeza mapato ya ndani kwa njia ya utalii. Kwani wapo watu wengi
kutoka nje ya nchi katika mataifa mbalimbali duniani hasa wanasayansi watakao
kuja nchini kwa lengo la kujionea tukio hilo.
Huu ni utalii wa anga. Hivyo wananchi wa Rujewa na
Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya hawana budi kuandaa mazingira ya kupokea ugeni
huo kwa kuwaandalia mazingira mazuri na ujuo huo ni wazi kuwa utaongeza pato la
taifa na wananchi wa Rujewa pia endapo watachangamkia fursa hiyo ya ugeni.
Ni vyema sasa vyombo husika ikiwepo serikali
kuanza kampeni ya kuhamasisha jamii za ndani na nje ya nchi kuweza kufika
katika eneo hilo Septemba mosi mwaka huu kujionea tukio hilo la kihistoria.
Wizara ya Maliasili na Utalii, pia inaweza kutumia
fursa hiyo kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika mikoa ya Kanda ya
Nyanda za juu kuzini kama vile, Hifadhi ya Taifa Kitulo, Hifadhi ya Ruaha na
hata Hifadhi ya taifa Mikumi.
Tanapa itumie fursa hiyo pia kuhamasisha watalii
kuja nchini na kwenda mkoani Mbeya kujionea kupatwa huko kwa jua kipete pamoja
na kutembelea vivutio vilivyopo katika ukanda huo.
Kufanya hivyo kutaifaidisha nchi kiuchumi kwa
kupata watalii kutoka nchi za nje ambao watakuja kushuhudia tukio hilo na
kuiingizia nchi fedha za kigeni.
Kampuni za utalii zinatakiwa zitumie fursa kwa
kutangaza kwa njia mbalimbali huduma zao na namna ya kuweza kufiskisha wageni Rujewa
kuangalia jua likipatwa kipete pamoja na fursa ya kutembelea hifadhi kama
Kitulo.
No comments:
Post a Comment