Afisa Mawasiliano Mwandamizi
wa TPA, Bw. Focus Mauki (kushoto) akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari
(hawapo pichani) kuhusu matumizi ya Mfumo mpya wa malipo wa Kelektroniki
kulipia huduma za Bandari. Mfumo huo wa malipo tayari umeanza kutumika tangu
mwezi Julai mwaka huu na umeongeza ufanisi wa Bandari na
kurahisisha kazi ya kutoa mizigo Bandarini. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa
TEHAMA wa Mamlaka, Bw. Kilian Challe na Afisa Habari wa Idara ya Habari
Maelezo, Bw. Frank Mvungi.
Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA wa
TPA, Bw. Kilian Challe akiwaeleza Waandishi wa Habari kuhusu mipango ya Mamlaka
kuanza kutumia huduma za simu za mkononi, Master Card na Visa kulipia gharama
za Bandari kwa kupitia mfumo wake mpya wa Malipo kwa njia ya Kielektroniki
(IePS). Kushoto ni Afisa Mawasiliano Mwandamizi TPA,
Focus Mauki na Afisa Habari kutoka Idara ya Habari Maelezo, Bw. Frank Mvungi.
************
Na Focus Mauki-TPA
Wateja wa Bandari ambao ni Mawakala wa kutoa mizigo Bandarini sasa
wataanza kutumia huduma za malipo kupitia njia za Simu za Mkononi, Visa Card na
Master Card wakati wa kulipia gharama za huduma Bandari.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA, Bw. Kilian Chale wakati
wa mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari
Maelezo Ijumaa, Oktoba 9.
“Napenda kuwatangazia wateja wetu na Watanzania wote kuwa katika siku
za karibuni Mfumo wetu wa Malipo kwa njia ya Kielektroniki (IePS) ambao tuliuzindua
Julai 2015 utaanza kuruhusu matumizi ya Master Card, Visa na simu za mkononi
katika kulipia huduma za Bandari,” amesema Kilian.
Kilian ametoa wito kwa Mawakala wa Mizigo Bandarini kuendelea na
usajili wa ktumia mfuo huu ili kurahisisha na kuharakisha kazi ya kutoa mizigo
Bandarini na kuongeza ufanisi wa Bandari katika kuhudumia wateja wake.
Tayari Mawakala wengi wameanza kutumia mfumo huu ambao tayari umeeunganishwa
na Benki za CRDB, NMB na Benki ya Posta ili kumwezesha Wakala kupata Ankara ya
malipo, kufanya malipo na kisha kwenda moja kwa moja katika eneo la kuchukulia
mzigo ndani ya Bandari.
Mpaka sasa Wakala anaweza kutumia Benki ya CRDB na NMB kufanya malipo
kwa kutumia CRDB Sim Banking, CRDB Internet Banking, CRDB fahari Huduma, NMB Internet
Banking, NMB Mobile Banking na pia anaweza kutumia matawi ya CRDB, NMB na Benki
ya Posta.
Ili kuweza kutumia mfumo huu wakala anapaswa kusajiliwa na Mamlaka na
baada ya kusajiliwa anaweza kuingia katika mfumo kupitia tovuti rasmi ambayo ni
www.tpapayments.com.
Mteja wa kawaida pia anaweza kuingia katika tovuti hii na kuweza kuona
Ankara ya malipo ya huduma za Bandari kwa kila mzigo au gari aliloagiza. Pamoja
na mambo mengine mfumo huu unatarajiwa kuweka uwazi na kupunguza kwa kiwango
kikubwa malalamiko ya wateja ya kukosa
taarifa sahihi za gharama za mizigo yao.
No comments:
Post a Comment