Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka
akitoa tamko la Serikali kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya
usitishwaji wa utaratibu wa kukodisha wafanyakazi unaofanywa na baadhi ya
mawakala binafsi wa huduma za ajira wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi
wa idara ya habari(MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.
******
1.Wizara ya Kazi na Ajira imekua ikipokea malalamiko toka kwa wadau mbalimbali utaratibu wa udalali wa kukodisha wafanyakazi
katika makampuni unaofanywa na baadhi ya Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira
nchini.
2.Wizara imefanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hili na
kubaini kuwa utaratibu wa kukodisha wafanyakazi unaofanywa na baadhi ya Wakala
Binafsi wa Huduma za Ajira ni kinyume cha Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya
Mwaka 1999 [Sura 243 kama ilivyorejewa Mwaka 2002].
Kwa mujibu wa Kifungu 4 cha Sheria hii, majukumu
ya msingi ya Wakala wa Huduma za Ajira ni kuwaandaa na kuwaunganisha Watafuta Kazi na Waajiri kwa kutoa
mafunzo na ushauri elekezi kwa watafuta
kazi, kutafuta fursa za ajira na kutoa
taarifa za soko la ajira. Hivyo,
Mawakala hawapaswi kuwa waajiri wa wafanyakazi waliowatafutia kazi kwa niaba ya
Waajiri wengine.
3.Aidha, uchunguzi umebaini kwamba utaratibu huu ni ujanja unaotumiwa na baadhi
ya Waajiri na Mawakala kwa lengo la kukwepa kodi na kujipatia faida kwa kukwepa
kutoa haki za msingi za wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria za Kazi. Baadhi ya
makampuni yanayokodisha wafanyakazi yamefanyiwa uhakiki na TRA na kubainika
kukwepa kodi ya mapato ya ajira (PAYE) na
na kodi ya mapato ya kampuni kinyume na Kifungu cha 7 cha Sheria ya Kodi
ya Mapato ya Mwaka 2004 [Sura 332 kama ilivyorejewa
Mwaka 2008].
4.Uchunguzi huu umebaini
athari mbalimbali kwa wafanyakazi wanaoajiriwa kwa utaratibu huu. Athari
hizo ni pamoja na:
·
Wafanyakazi kukosa haki ya hifadhi ya jamii kama vile likizo ya uzazi na
matibabu kinyume na Sheria mbalimbali za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii;
· Uwepo wa ubaguzi katika malipo ya mishahara kwa kazi
ya aina moja kinyume na kifungu cha 7(10) cha Sheria ya Ajira na
Mahusiano Kazini Na.6 ya mwaka 2004 ambacho kinamtaka mwajiri kuchukua hatua
stahiki kwa kuhakikisha kuwa wafanyakazi bila kujali jinsia zao wanalipwa
mishahara linganifu na ya haki kwa kazi yenye uzito na thamani sawa;
·
Kukosa fursa za kujiendeleza kielimu na mafunzo;
·
Kukosekana kwa usalama na uhakika wa ajira ;
· Wafanyakazi kulipwa mishahara ya kima cha chini kinyume na
sekta wanayofanyia kazi.
5.Kwa taarifa hii, Wizara ya Kazi na Ajira
imeamua kusitisha mara moja utaratibu wa Mawakala kuwaajiri wafanyakazi wanaowatafutia kazi.
Aidha,Mawakala na Kampuni husika waliopo katika utaratibu huu kwa sasa
wanapaswa kuwahamisha wafanyakazi
waliokodishwa
kutoka kwa Wakala kwenda kwa Kampuni husika. Waajiri na Wakala wanatakiwa
kukamilisha zoezi hili ndani ya kipindi cha mwezi mmoja na kuwasilisha taarifa
za utekelezaji kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Kazi na Ajira kabla au ifikapo tarehe
28/02/2014.
6.Uchunguzi zaidi unaendelea kubaini kama kuna wafanyakazi
wa Kigeni wanaohusishwa katika utaratibu wa kukodishwa ili hatua zinazotahili
ziweze kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwataka waombe vibali vya ajira kwa
mujibu wa Sheria ya Uhamiaji Na.7 ya mwaka 1995 na Sheria ya Huduma za Ajira Na.9
ya mwaka 1999. Wageni watakao kidhi vigezo wataajiriwa na kampuni
walipokodishwa; ambazo kwa wakati huo zitakua ndiyo mwajiri wao.
7.Wizara ya Kazi na Ajira inawaelekeza Wakala wa Huduma
za Ajira nchini kwamba, kwautaratibu wa sasa watapaswa kuwasilisha barua za
maombi ya usajili wa Uwakala kwa KAMISHNA WA KAZI
kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya mwaka 1999 [Sura 243
kama ilivyorejewa Mwaka 2002] ili waweze kufanya shughuli za Uwakala wa Huduma
za Ajira kisheria. Maombi haya yawasilishwe ndani ya kipindi cha mwezi mmoja
tangu kutolewa kwa tangazo hili. Baada ya muda huo Wakala asiye na kibali cha Kamishna
wa Kazi hatoruhusiwa kuendesha shuguli za huduma za ajira nchini.
Aidha, Mawakala watakaopata leseni ya Kamishna wa
Kazi yatakua yakitangazwa ili yatambuliwe na Umma.
8.Nasisitiza, maelekezo haya yatatolewa kwa
Makampuni na Wakala waliohusishwa katika
uchunguzi kwa ajili ya utekelezaji.
IMETOLEWA NA
GAUDENTIA MUGOSI KABAKA
(MB)
WAZIRI WA KAZI NA AJIRA
27/01/2014
No comments:
Post a Comment