January 10, 2014

KESI YA BOSI WA ZAMANI WA TBS CHARLES EKEREGE ILIVYOENDELEALEO MAHAKAMANI KISUTU

 
 Aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekerege  na binti yake wakiondoka katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana kusikiliza mwenendo wa kesi yake ya matumizi mabaya ya madaraka  kwa kutoa asilimia 50 ya punguzo la tozo ya utawala kwa Kampuni mbili na kulisababishia TBS hasara ya Dola 42,543 za Kimarekani.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekerege (kulia) na familia yake akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana kusikiliza mwenendo wa kesi yake ya matumizi mabaya ya madaraka  kwa kutoa asilimia 50 ya punguzo la tozo ya utawala kwa Kampuni mbili na kulisababishia TBS hasara ya Dola 42,543 za Kimarekani. 
**********
 MASHAHIDI wa Jamhuri katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekerege (pichani) ya matumizi mabaya ya madaraka  kwa kutoa asilimia 50 ya punguzo la tozo ya utawala kwa Kampuni mbili na kulisababishia TBS hasara ya Dola 42,543 za Kimarekani, wamedai kwa nyakati tofauti kwamba mshtakiwa alitoa msamaha huo bila kibali cha Baraza la Utendaji (kwa sasa Bodi ya Wakurugenzi). 
 
 Mashahidi hao wa kwanza Mwansheria Batista Bitao na wa pili ni Mhandisi Joshua Katabwa walitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam. 
 
 Akiongozwa na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Janeth Machulya shahidi huyo alidai kuwa katika kipindi cha mwaka 2007 na 2009, kwa mujibu wa mikataba ya TBS na Kampuni ya Jaffar Mohamed Ali Garage ya nchini Dubai na Quality Motors ya Hongkong walipaswa kulilipa shirika hilo asilimia 25 baada ya kufanya ukaguzi. 
 
 Alidai kuwa kati ya mwaka 2007 na 2009, Baraza la Utendaji (kwa sasa Bodi ya Wakurugenzi) ni chombo pekee chenye dhamana ya kusimamia shirika hilo.
 
 “Mwaka 2007 na 2009 nilikuwa naalikwa katika baraza la utendaji (Bodi ya Wakirugenzi) lakini hatukuwahi kujadili suala la kusitisha tozo ya ada ya utawala… suala hilo liliibuka mwaka 2011 baada ya menejimenti kuwasilisha taarifa ya kutolewa msamaha kwa kampuni hizo mbili na iliambatanisha na maelezo ya kuomba radhi kuhusu kosa la kutoa msamaha huo bila kibali cha baraza hilo na kwamba halitajirudia,” alidai Bitao. 
 
Akifafanua zaidi alidai kuwa baraza hilo lilitoa maelezo yake kwamba kosa hilo sijirudie tena na kwamba menejimenti baada ya kupitia maombi hayo ilipaswa kuyawasilisha katika baraza hilo ili liweze kutoa uamuzi wa kukubali au la. 
Naye shahidi wa pili, Katabwa alidai kuwa kampuni hizo ziliingia mkataba na shirika lake kwa mkataba wa kulilipa asilimia 25 na kampuni hizo kubaki na asilimia 75 kama wakala wao. Alidai kuwa Machi 28, mwaka 2008 aliagizwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa TBS (wakati huo, Ekerege) kuandaa barua ya kutoa msamaha wa asilimia 50 kwa kampuni ya Jaffar Mohamed Ali Garage. 
 
 “Ekerege aliniagiza niandae barua ya kuwakubalia msamaha huo na aliisaini tarehe hiyo waliyowasilisha maombi yao… utaratibu huo ulitumika kwa kampuni ya Quality Motors kupokea majibu ya msamaha huo” alidai Katabwa.
 
 Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Machi 28 mwaka 2008 na Agosti 7, mwaka 2009, katika ofisi za TBS iliyopo wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu Ekerege alitumia madaraka yake vibaya. 
 
 Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa punguzo la asilimia 50 ya ada ya utawala kwa kampuni hizo bila idhini ya baraza la utendaji la TBS kinyume cha sheria namba 2 kifungu kidogo cha (3) ya TBS ya mwaka 2005. 
 
 Ilidaiwa kuwa kitendo hicho kiliziongezea kampuni hizo faida ya Dola 42,543 za Kimarekani sawa na (kwa wakati huo) Sh. Milioni 68,068,800. 
 
 Upande huo wa Jamhuri ulidaiwa shitaka la pili, katika tarehe na mahali pa tukio la kwanza, mshtakiwa alilisababishia shirika kupata hasara ya fedha hizo. 
 
 Mshtakiwa alikana mashitaka yote mawili na yuko nje kwa dhamana na kesi hiyo itaendelea kusikilizwa mfululizo Februari 5,6 na 7, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment