December 11, 2013

TAMKO LA WENYEVITI WA CCM-MIKOA LA KUMPONGEZA KATIBU MKUU WA CCM NDG. ABDULRAHAMAN OMAR KINANA NA SEKRETARIETI YA CCM TAIFA.

10 
Mgana Izumbe Msindai – Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM wa Mikoa akitoa tamko hilo kwenye makao makuu ya Chama Chama Mapinduzi Ofisi ndogo Lumumba jijini Dar es salaam leo,kulia ni Haji Juma Haji – Makamu Mwenyekiti Wa Wenyeviti Mikoa na kushoto ni Lucas Ole Mukusi – Katibu wa Wenyeviti Mikoa.
***********
Sisi Wenyeviti wa CCM-Mikoa tuliokutana leo, Desemba10/2013 hapa Dar es salaam, kwa kauli moja na kwa niaba ya wanaCCM wa mikoa yetu, tunatoa kauli ya kumuunga mkono Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi ndugu Abrahamani Kinana na Sekretarieti yote kwa utekelezaji uliotukuka wa majukumu yao ya kichama.

Tangu alipopewa wadhifa wa Ukatibu Mkuu ameonyesha uwajibikaji mkubwa, uliokiwezesha Chama kupata uhai mpya na kuamsha Ari na matumaini zaidi ya Watanzania kwa Chama Cha Mapinduzi.

WanaCCM nchini tuko katika mstari wa mbele kuisimamia Serikali yetu kwa mujibu wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015 sura ya Tisa; Inayokitaka Chama kuisimamia Serikali yake.

Kwa pamoja tunaungana na kupinga kwa nguvu zote mambo yafuatayo;  

1. Ubadhirifu unaofanywa katika Serikali za Mitaa nchini unaozifanya Halmashauri nyingi kujirudiarudia kupata hati chafu na zenye mashaka, inayosababisha hasara na manung’uniko kwa wananchi.  

2. Utelezaji duni wa baadhi ya miradi ya maendeleo unaopelekea kuwepo kwa huduma duni na zisizokidhi thamani ya fedha na matakwa ya kitaalamu. Hii inaashiria uwepo wa Rushwa na ubadhirifu wa fedha kwa baadhi ya miradi ya maendeleo. 

3. Ucheleweshaji wa maslahi na stahiki za watumishi wa Umma kunakopelekea kuwa wavunja moyo na ari watumishi, katika kutekeleza majukumu yao na hivyo kusababisha kutokea kwa migomo ya mara kwa mara kufuatia uzembe katika kuwapatia haki zao, kinyume na misingi ya utawala bora.  

4. Gharama kubwa ya uendeshaji wa shughuli za Serikali na Taasisi zake ikilinganishwa na gharama zinazotumika kwenye miradi ya maendeleo na uboreshwaji wa huduma za jamii kwa wananchi.  

5. Usimamizi mbovu wa Operation mbali mbali za Serikali zenye nia njema kwa Taifa. Mfano Operasheni kuhamisha wafugaji na Operasheni Tokomeza; Zina nia njema lakini usimamizi wake umekuwa mbovu hata kupelekea kuvuruga nia yake njema kwa Taifa. 

 6. Kushindwa na Kuchelewa kutatua baadhi ya Kero sugu kwa Wananchi kama malalmiko mbali mbali ya wakulima (mfano mbolea za minjingu kutofanya vizuri kwa asilimia kubwa, matatizo ya wakulima wa pamba na korosho nk.) na wafugaji; Rushwa zilizokithiri katika sehemu mbali mbali za utoaji wa huduma kwa wananchi na ucheleweshwaji wa fadha za miradi ya maendeleo nk.

Katibu Mkuu wa CCM daima amekuwa akikemea kwa nguvu zote madhaifu yote tuliyoyataja hapo juu na sisi kama Wenyeviti wa CCM Mikoa yote Tanzania. Tunaitaka Serikali ichukue hatua za haraka katika kurekebisha madhaifu hayo.
Viongozi na watendaji wengine wote wa Serikali, walioonesha udhaifu mkubwa katika kutekeleza majukumu yao, na ambao walipewa wito na wengine ambao wanatakiwa kupewa wito; wa kuhudhuria mbele ya Kamati Kuu ya CCM wachukuliwe hatua zinazostahili.

Tunawakumbusha viongozi wa Serikali watambue kuwa Chama cha Mapinduzi kinaisimamia Serikali kwa mujibu wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015 Sura ya Tisa. 
  _______________________________________________ 
Mgana Izumbe Msindai – Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM wa Mikoa ___________________________________________________ 
Haji Juma Haji – Makamu Mwenyekiti Wa Wenyeviti Mikoa __________________________________________  
Lucas Ole Mukusi – Katibu wa Wenyeviti Mikoa

No comments:

Post a Comment