Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa
taarifa ya tukio la leo, Jumapili, Mei 5, 2013 la mlipuko kwenye Kanisa
Katoliki la Mt. Joseph Mfanyakazi la Olasiti Jijini Arusha.
Tukio hilo la kigaidi limesababisha mtu mmoja
kupoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa.
Rais Kikwete analaani vikali shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu
katili, waovu na wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa Tanzania na watu
wake.
Rais Kikwete ameagiza vyombo
vya usalama nchini kumsaka mtu au watu waliohusika na kitendo hicho kiovu na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Vile
vile Rais Kikwete amewataka wananchi wote kuwa watulivu wakati Serikali na
vyombo vyake inaendelea kufuatilia tukio hili.
Tutawasaka popote walipo na kupambana
nao bila huruma. Aidha, tutakabiliana na
aina yoyote ya uhalifu nchini iwe ni ugaidi au aina yoyote ya uhalifu wa namna
hiyo au wa namna nyingine, uwe na chimbuko lake ndani ya nchi ama nje ya nchi
yetu.
Kamwe hatutakubali kuwaacha
wavuruge amani na usalama wa Tanzania na watu wake. Rais anaamini kuwa Serikali,
kwa msaada na ushirikiano wa wananchi, watu hao watapatikana na kuadabishwa
ipasavyo.
Aidha, Rais Kikwete anatoa rambirambi
za dhati ya moyo wake kwa wafiwa na wale wote ambao wamejeruhiwa katika tukio
hilo. Anaungana nao katika machungu na msiba. Rais pia anawaombea wote
walioumia katika tukio hili wapate nafuu ya haraka na waendelee na shughuli zao
za ujenzi wa taifa.
Rais Kikwete vilevile anatoa
pole nyingi kwa viongozi na waumini wa Kanisa Katoliki kwa tukio hili la
kusikitisha na kuvurugika kwa ibada na shughuli yao muhimu ya uzinduzi wa
Kanisa lao.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
5 Mei, 2013
No comments:
Post a Comment