Na
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI
kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema haitabidili kamwe
maamuzi iliyotoa kuhusu Pori Tengefu la Loliondo, mkoani Arusha na kuwataka
wanaharakati wanaochochea mgogoro wa ardhi katika eneo hilo kuacha mara moja.
Tamko hilo la serikali, limekuja muda mfupi baada ya watu mbalimbali kutoa maoni yao kwenye mitandao na vyombo vya habari kwamba uamuzi wa serikali kuhusu pori tengefu si sahihi.
Tamko la serikali lilitangazwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki hivi karibuni kwamba, wameacha kilomita za mraba 25,000 kwa ajili ya wananchi na serikali imechukua kilomita za
mraba 15,00 kwa ajili ya kutunza rasilimali za nchi.
Alifanya hivyo kwa kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009, Sehemu ya 16 Vifungu Na. 4, 5 na 6 na kwamba muda mrefu viongozi wa wizara wamekuwa wakikutana na wananchi na viongozi wa mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro kujua kero zilizopo ili zitatuliwe na ndio imewezesha serikali kufanya uamuzi alioufanya.
"Ukweli ni kuwa Waziri Kagasheki alifuata sheria alipotoa tamko kuhusu kupunguza eneo la pori tengefu la Loliondo kwa mujibu wa sheria inayompatia waziri mwenye dhamana uwezo wa kupitia upya mapori tengefu na kufanya marekebisho mbalimbali muhimu kwa manufaa ya wananchi bila kuathiri hifadhi,"alisema George Matiko, ambaye ni msemaji wa wizara.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari jana, Matiko alisema tamko lilizingatia tafiti mbalimbali ikiwemo utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) na mapendekezo ya tume mbalimbali ilizoundwa kuchunguza mgogoro wa Loliondo ikiwemo ya Waziri Mkuu iliyoundwa mwaka juzi.
Aliongeza kuwa eneo la kilomita za mraba 1,500 litaendelea kumilikiwa na wizara kwa mujibu wa sheria na kwa kutambua kuwa ni sehemu ya mazalia ya wanyamapori, mapito ya wanyamapori na vyanzo vikuu vya maji kwa hifadhi mbalimbali ikiwemo Serengeti.
Alisisitiza ardhi iliyobaki baada ya kuondoa eneo la pori tengefu la Loliondo itasimamiwa na vijiji kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya Mwaka 1999 na wananchi watawezeshwa ili waanzishe Eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) katika ardhi hiyo kwa manufaa yao.
"Tanzania inajali uhifadhi lakini pia inajali maslahi ya wananchi, ndiyo maana asilimia 25 ya eneo la nchi hii limehifadhiwa bila kuwepo migogoro. Hakuna migogoro kati ya wananchi na Serikali, kwa kuwa wananchi wanatambua umuhimu wa uhifadhi kwao na kwa vizazi vijavyo. Ndiyo maana wananchi wanachangia kwa kiwango kikubwa katika kufanikisha uhifadhi,"alimaliza Matiko.
No comments:
Post a Comment