December 16, 2012

Tamko La Vijana Wa CHADEMA Mkoa Wa Mwanza

KWA nafasi yangu ya Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) Mkoa wa Mwanza, nimelazimika kutoa ufafanuzi na kuweka kumbukumbu sawa na kutuliza munkari ya vijana wa mkoa huu na nchi nzima kutokana na habari zilizosambazwa kwa njia mbalimbali za upashanaji habari.

Imeripotiwa katika njia hizo za upashanaji habari kuwa BAVICHA wanataka Katibu Mkuu wetu wa Chama, Dkt. Willibrod Slaa, aondoke madarakani na kwamba asipoondoka, wataandaa mandamano ya kumng’oa.

Napenda kutumia nafasi hii kusema maneno machache juu ya upuuzi huo ambao kilamtu anajua umetokana, unaratibiwa na kusimamiwa na CCM, ikiwa eti ndiyo moja ya mikakati ya Sekretarieti ya chama hicho inayoitwa kuwa ni mpya.

Kwa nafasi yangu, mimi ndiye msemaji mkuu wa masuala yote yanayohusu BAVICHA kwa mkoa wa Mwanza. Kwa mamlaka yangu ninaelewa fika vijana wa Mwanzahawajawahi, wala hawana mpango wa kubeba propaganda za CCM dhidi ya CHADEMA na viongozi wetu kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu, akiwemo Katibu Mkuu,Dkt. Slaa.

Natumia fursa hii kuwaondolea wasiwasi vijana wa CHADEMA mahali kokote ndani na nje ya nchi, vijana wa Mwanza tuko imara kukilinda chama chetu na viongozi wetu dhidi ya propaganda za CCM na serikali ambazo zina lengo ya kudhoofisha harakati za kujenga taasisi imara inayobeba matumaini ya Watanzania kwa ajili ya ukombozi wa awamu ya pili.

Natumia nafasi hii pia kuwataka vijana wa CHADEMA Mkoa wa Mwanza watulie, wakisubiri BAVICHA Mkoa ifanye maamuzi kwa kuzingatia maslahi mapana ya umma wa Watanzania na chama chetu dhidi ya hila, njama na uchu wa mtu mmoja mmoja miongoni mwetu ambaye anaamua ‘kufika bei’ na kubeba propaganda za CCM.

Napenda kuwaambia vijana wa CHADEMA kuwa mapambano ambayo chama chetu kinayaendesha kiasi cha kutishia CCM kuendelea kuwepo madarakani mwaka 2014 na 2015, ni mapambano ya haki dhidi ya udhalimu, ni mapambano ya matumaini dhidi ya kukataa tama, ni mapambano ya uadilifu dhidi ya ufisadi.

Katika kusimamia masuala hayo, Katibu Mkuu CHADEMA, Dkt. Slaa akiwa mtendaji mkuu wa chama amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha CCM inadhoofika kabisa na CHADEMA inaendelea kuwa tumaini jipya la huru wa kweli, mabadiliko ya mfumo na utawala, baada ya uchaguzi mkuu 2015.

Vijana wa Mwanza, kama walivyo vijana wote walio wanachama makini wa CHADEMA, tunatambua Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992, inayosimamia shughuli zote za vyama vya siasa nchini inasema wazi mtu aliyekuwa mwanachama wa chama X akiamua kujiunga chama Y, ‘automatically’ anapoteza uanachama wa chama cha awali.

Lakini pia tunatambua kuwa katiba za vyama vya siasa, ikiwemo Katiba ya CCM, zinasema wazi kuwa mwanachama wa chama hicho akijiunga na chama kingine, anapoteza uanachama wake kwa chama hicho cha awali automatically.

Lakini pia vijana wa CHADEMA Mwanza ambao ni makini kama ilivyo kawaida ya vijana wa CHADEMA, tunaelewa wazi na tunaweza kusimamia kauli hii, kuwa Katibu Mkuu Dkt. Slaa tangu alipohama CCM mwaka 1995 hajawahi, kwa maana ya kila mwaka, kwenda ofisi yoyote ya CCM kulipia kadi yake kuhuisha uanachama kwenye chama hicho alichokiacha kinachokufa, kikisubiri kuzikwa rasmi mwaka 2014 na 2015.

Tunatambua kwamba Dr Slaa ni mwachama hai wa CHADEMA na si mwanachama wa CCM.

Kwa namna anavyofanya kazi zake, tangu akiwa bungeni, namna alivyotaja “orodha ya mafisadi (list of shame) iliyohusisha viongozi wa Serikali na CCM, alivyoombwa kugombea urais na kuungwa mkono na watanzania, anavyosimamia utendaji wa CHADEMA na kuhakikisha chama chetu kinatekeleza wajibu wake katika kila jukwaa dhidi ya serikali ya CCM, ni kijana mpuuzi na msaliti anaweza kusimama kumnyooshea kidole kwa kutumia propaganda za CCM na vibwagizo vya Nape Nnauye na CCM.

Natangaza rasmi kuwa BAVICHA Mwanza haijafanya maamuzi ya kuendesha harakati

zozote za kutaka Dkt. Slaa ajiuzulu, wala haitambui maandalizi ya maandamano

kwani ni batili na aliyetoa tamko la jana, Salvatory Magafu si msemaji wa vijana wa

CHADEMA Mkoa wa Mwanza, na hivyo baraza litakaa kujadili utovu huu wa nidhamu

wa kiwango na kuchukua hatua stahiki.

BAVICHA Mwanza inaheshimu taratibu za kikatiba wa viongozi kutokutuhumiana

kwenye vyombo vya habari, hivyo nimetoa kauli yangu kama Msemaji wa BAVICHA

ngazi ya Mkoa hapa Mwanza ili kuweka kumbukumbu sahihi kwa umma na maamuzi

mengine yataendelea kufanywa kwa mujibu wa katiba, kanuni, maadili na itifaki ya

chama.

Liberatus B. Mulebele.

Mwenyekiti wa BAVICHA Mkoa wa Mwanza.

No comments:

Post a Comment