November 21, 2012

TIKETI ZA FAINALI ZA AFCON 2013 KUPATIKANA KWA MTANDAO

Washabiki wanaotaka kushuhudia Fainali za 29 za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Januari mwakani nchini Afrika Kusini watapata tiketi kwa njia ya mtandao.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) tiketi kwa ajili ya washabiki (public tickets) wanaotaka kuhudhuria fainali hizo zitakazoanza Januari 19 na kumalizika Februari 10 mwaka huu, zitauzwa kupitia mtandao wawww.afcon2013booking@eqtickets.com. Pia tiketi zitapatikana kupitia simu namba+27 879803000.

Fainali hizo zinazoshirikisha timu 16 zitachezwa Johannesburg, Nelson Mandela Bay, Mbombela, Durban na Rustenburg. Mechi ya fainali itachezwa Februari 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Soccer City jijini Johanesburg kuanzia saa 2 usiku kwa saa za Afrika Kusini.

Mechi ya ufunguzi wa fainali hizo itachezwa Januari 19 mwaka huu ambapo wenyeji Afrika Kusini (Bafana Bafana) wataumana na Cape Verde kuanzia saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Soccer City.

Angola na Morocco zitacheza mechi ya pili kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 3 usiku. Timu zote hizo ni za kundi A. Mabingwa watetezi Zambia wako kundi C na wataanza mechi yao ya kwanza Januari 21 mwaka huu dhidi ya Ethiopia saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Mbombela. Timu nyingine katika kundi hilo ni Nigeria na Burkina Faso.

No comments:

Post a Comment