July 23, 2008

TID aifuata familia ya babu Seya Segerea

MSANII maarufu wa muziki wa kizazi kipya (Bongofleva), Khalid Mohamed maarufu kama T.I.D (pichani) amehukumiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela kufuatia kupatikana na hatia ya kushambulia na kujeruhi.

T.I.D mwenye umri wa miaka 26 alisomewa adhabu yake hiyo na Hakimu Hamisa Kalombola wa Mahakama ya wilaya ya Kinondoni baada ya Hakimu huyo kuridhika na ushahidi ulitolewa na mashahidi wanne walioletwa mahakamani na upande wa mashtaka.

Baada ya kusikiliza ushahidi huo, ndipo Hakimu Kalombola alisema ushahidi uliotolewa na mashahidi hao wanne ulithibitisha mtuhumiwa kufanya kosa hilo na hivyo mahakama inamtia hatiani kwa kosa hilo.

Mara baada ya kusema hivyo Hakimu alitoa nafasi kwa Mwendesha Mashtaka, Inspekta wa Polisi, Benedict Nyagabona ambaye alimwomba Hakimu kutoa adhabu kali kutokana na tabia iliyokithiri ya watu kujichukulia sheria mkononi kama alivyofanya mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Baada ya maelezo hayo ya Mwendesha Mashtaka ndipo Hakimu alitoa nafasi kwa mshtakiwa TID kutoa utetezi wake, ambaye aliiomba mahakama imhurumie kwani alitenda kosa hilo sababu ya ulevi na kuwa familia yake inamtegemea hasa mama yake.

Hata hivyo Hakimu Kalombola alitoa hukumu hiyo kwa kumwambia mshtakiwa “kwa vile huwezi kujimudu ukilewa na huwezi kujizuia kunywa sasa na kuhukumu uende jela mwaka mmoja ujifunze ili usiwe unakunywa hizo pombe”

Baada ya hukumu hiyo ambayo ilipokelewa kwa mshtuko mkubwa na msanii huyo aliyeng’ara sana katika fani hiyo ya muziki wa Bongofleva akiwa na bendi yake ya Top Band, ndugu na jamaa zake waliangua kilio mahakamani hapo wakati TID akipelekwa kwenye karandinga tayari kwenda kutumikia kifungo hicho katika gereza la Segerea.

Wakati akipelekewa kwenye karandinga hilo, TID aliishiwa nguvu na kuanguka mahakamani hapo na kubebwa na wenzake ambao baadhi yao walikuwa wamekwisha hukumiwa na wengine bado wakiwa watuhumiwa na kumwingiza kwenye gari hilo.

Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka, Inspekta Nyagabona, T.I.D alimjeruhi Ben Mashiba kichwani na mkononi kwa kutumia chombo cha kuwekea majivu ya sigara ‘Ash Tray’ na alisomewa mashtaka hayo mara ya kwanza Julai 10 mbele ya Hakimu Kalombola.

Mwendesha Mashtaka huyo aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Julai 2 mwaka jana saa sita na nusu usiku katika hoteli ya Slipway iliyopo maeneo ya Msasani jijini Dar es Salaam .

5 comments:

  1. AnonymousJuly 24, 2008

    Ben Machiba anasababu nyingine kabisa kupigwa na ash tray kweli umuweke mwenzako ndani? Mbona watu wanachomana visu kesi inaisha kwa maelewano kati yenu.
    Mungu atakulinda TID nenda tu. Na huyo Ben Machiba atahukumiwa na kesi kubwa.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 24, 2008

    Kujeruhiwa tu???

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 24, 2008

    Na wewe Kidevu, kuandika kuwa TID aifuata familia ya babu Seya Segerea unaona raha eeh!!

    ReplyDelete
  4. AnonymousJuly 24, 2008

    Fundisho kwa wengine. Pombe si Chai

    ReplyDelete
  5. AnonymousJuly 24, 2008

    Mwaka mmoja ni muda mfupi sana vumilia TID tutakuja kukuona washkaji

    ReplyDelete