July 28, 2008

Mbunge wa Tarime Chacha Wangwe afariki dunia


MBUNGE WA TARIME (CHADEMA) CHACHA WANGWE (PICHANI) AMEFARIKI DUNIA KWA AJALI YA GARI ILIYOTOKEA MAJIRA YA SAA MBILI USIKU ENEO LA KONGWA, MKOANI DODOMA.KWA MUJIBU WA HABARI HIZO MAREHEMU WANGWE, AMBAYE ALIKUWA AMETOKEA BUNGENI DODOMA AMBAKO ALIHUDHURIA KIKAO CHA ASUBUHI, ALIKUWA NJIANI KUELEKEA DAR KWENYE MAZISHI YA HAYATI MZEE BHOKE MUNANKA AMBAYE AMEFARIKI DUNIA JUMAMOSI HII, AMBAPO LEO ANATARAJIWA KUZIKWA KWENYE MAKABURI YA KINONDONI, DAR ES SALAAM.AIDHA HABARI ZA KIFAMILIA ZINASEMA MAREHEMU JANA ALIKUWA ANAUMWA NA WATOTO WAKE WALIMSII ASISAFIRI AMBAPO PIA GARI LAKE HILO LILILIKUWA NA MATATIZO YA NATI KATIKA MAGURUDUMU YAKE NA ILIDAIWA KULIPRELEKA GEREJI KWA MATENGENEZO.MAREHEMU AMEACHA WATOTO 9 MWILI WA MAREHEMU UMEHIFADHIWA KATIKA HOSPITALI YA MKOA WA DODOMA.BUNGE LIMEAHIRISHA KIKAO CHAKE LEO KUOMBOLEZA KIFO HICHO.KWANIABA YA WADAU WOTE WA FATHER KIDEVU BLOG NATOA MKONO WA POLE KWA WAFIWA. MOLA AIWEKE ROHO YA MAREHEMU MH. CHACHA WANGWE MAHALI PEMA PEPONIAMINA

SOMA HAPA KWA MAELEZO ZAIDI.
Mbunge wa Tarime kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chacha Zakayo Wangwe (52)(PICHANI) .Wangwe, mmoja wa wabunge machachari na matata, alikufa jana saa 2:55 usiku kwa ajali ya gari akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda jijini Dar es Salaam kuwahi mazishi ya mmoja wa maveterani Bonke Mnanka ambaye anatarajiwa kuzikwa leo mchana katika makaburi ya Kinondoni.Spika wa Bunge, Samuel Sitta na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Omari Mganga, walithibitisha jana usiku kifo cha Wangwe ambacho kimetokea mwezi kamili tangu asimamishwe wadhifa wake wa Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema na siku moja kabla ya kesi yake ambayo ilitarajiwa kufanyika leo mahakama kuu.Kamanda Mganga alisema Wangwe alifariki dunia saa hizo eneo la Pandambili lililopo kati ya miji ya Kibaigwa na Gairo katika Barabara Kuu ya Dodoma – Morogoro wakati gari lake aina ya Toyota Corolla kupata ajali. Eneo hilo lipo wilaya ya Kongwa. Alisema ingawa chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika, lakini gari la mbunge huyo limeharibika vibaya, kwani limepasuka matairi yote ya mbele na nyuma kulia.Alisema Wangwe alikuwa katika gari hilo pamoja na rafiki yake, mfanyabiashara Deus Francis Mallya ambaye amepata majeraha madogo.Kufikia saa nne usiku jana, taarifa za kifo chake zilikuwa zimeanza kuenea katika kona ya mitaa ya mji wa Dodoma, kabla ya kuenea nchi nzima baada ya televisheni kadhaa na redio nchini kukatisha matangazo yao na kutangaza msiba huo.Kamanda Mganga amesema mwili wa Wangwe ulikuwa umehifadhiwa katika Zahanati ya Kibaigwa kabla ya kwenda kuuhamishia katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, tayari kwa taratibu nyingine za mazishi.Alisema wabunge wote wa Chadema walikuwa wamekusanyika jana usiku nyumbani kwa marehemu eneo la Kisasa kupanga taratibu za kumzika mwanasiasa huyo ambaye jina lake limevuma kwa kasi katika miaka michache aliyojihusisha na siasa.Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, akizungumzia kifo hicho alisema: “Tumeshitushwa sana, tumehuzunika sana. Kifo cha Wangwe kimenishitua sana, tulikuwa naye Wangwe asubuhi bungeni. Kwa kweli ni kama miujiza.”Kwa upande wake, Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohammed alisema kifo cha Wangwe ni pigo kubwa na kimemshitua sana, kwa sababu michango ya mbunge huyo ndani ya Bunge ilikuwa ya kuhamasisha na kujenga nchi.Ndani ya Bunge, Wangwe alikuwa akifahamika kama mmoja wa wabunge waliokuwa na mchango mkubwa na waliokuwa wakisikilizwa na wenzake kila aliposimama kutoa hoja.Alikuwa ni mwepesi wa kutoa hoja, lakini wakati mwingine zilimweka katika wakati mgumu bungeni kwa sababu zilikuwa zikikiuka Kanuni za Bunge, hivyo kuwalazimisha wabunge wenzake hasa wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumtaka kuthibitisha.Aliwahi kutakiwa na Spika Sitta kwa mujibu wa Kanuni, kuthibitisha madai yake kuwa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2005 jimboni mwake zilitawaliwa na ghasia za kisiasa kwa nia ya kumzuia kuwa mbunge wa jimbo hilo la Mkoa wa Mara.Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge ilichunguza na tuhuma hizo na kugundua kuwa si za kweli, hivyo Wangwe alionywa kwa kuwa hilo lilikuwa kosa lake la kwanza na kutakiwa kuwa makini na kauli zake zinazoweza kumletea matatizo siku za baadaye.Wangwe pia alitakiwa kuomba radhi bungeni.Kama hiyo haitoshi, Wangwe aliwahi kuingia matatani baada ya kudai bungeni kuwa baadhi ya vyombo vya umma, ikiwamo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), vinafanya kazi kwa maelekezo na kumpendezesha Rais.Katika kikao kimojawapo cha Bunge mwaka jana, wakati huo Dk. Batilda Burian akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), alimtaka mbunge huyo kuacha kumjadili Rais wa Jamhuri kwa kuwa sheria na Kanuni za Bunge haziruhusu.Katika suala hilo, alipotakiwa na mwenyekiti wa kikao, Jenista Mhagama kuomba radhi, badala ya kufanya hivyo, Wangwe alitoa maelezo kadhaa kuhusu kile alichokuwa akikijadili mwanzo, kisha aliomba radhi huku akitamka ‘lakini massage sent,’ kwamba ujumbe umefika.Kutokana na utata wa michango yake, alipachikwa jina la utani la ‘Unguided missile’, ambalo kwa tafsiri isiyo rasmi ni ‘kombora lisilokuwa na muongozaji’.Lakini atakumbukwa kwa tukio la hivi karibuni, baada ya kusimamishwa nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Juni 28, mwaka huu baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kutangaza uamuzi huo uliopingwa na mbunge huyo matata.Wakati akitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari Juni 29, mwaka huu, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, alidai tuhuma zilizomkabili Wangwe ni kushindwa kutekeleza majukumu yake pamoja na kushindwa kushirikiana na uongozi wote wa chama ngazi ya Taifa na Sekretarieti yake.Lakini Wangwe alijibu mapigo, akisema atakata rufani kwa Baraza Kuu na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa chama hicho atajitokeza kuwania nafasi ya uenyekiti inayoshikiliwa na Mbowe.Wangwe alisema Chadema imegubikwa na ukabila, fedha za ruzuku hazifiki kwenye majimbo na zinaishia makao makuu ya chama hicho na upendeleo katika ajira za chama hicho.Makubo Haruni aliyeko Tarime, anaripoti kuwa wananchi wa huko jana usiku walipokea kwa mshtuko habari za kifo cha mbunge huyo machachari.Alisema wengi wanamkumbuka kwa jinsi alivyokuwa akiwachachafya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime katika vikao vya madiwani na hata wa Serikali Kuu ingawa alikuwa ‘mtu wa ngumi mkononi’ hadi majukwaa ya wapinzani wake kisiasa.“Watakukumbuka jinsi kesi nyingi zilizvyomwandama na wakati fulani akahukumiwa kwenda jela miaka mitano ingawa baadaye aliachiwa huru baada ya kusaidiwa huduma ya uwakili na Tundu Lissu,” alisema Makubo.Kwa mujibu wa mwandishi huyo, jingine ambalo Wangwe atakumbukwa nalo ni hatua yake ya kuendelea kuwa Diwani kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi kwa miaka takribani miwili wakati tayari alikuwa amehamia Chadema.Ndugu zake wengine ni pamoja na Profesa gwiji wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Samwel Wangwe na Peter Wangwe, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime kwa tiketi ya CCM kwa miaka 15 na walikuwa wakichachafyana kisiasa wakati marehemu akiwa Diwani.Ndugu hao wawili nusura wakabiliane kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubunge kwa tiketi za vyama tofauti mwaka 2005 kama Peter Wangwe asingeangushwa katika kura za maoni.Chacha alishinda uchaguzi huo kwa kura nyingi katika kinachoaminika kwamba alitumia mwanya wa wananchi kutoridhishwa na chaguo la CCM na vyama vingine la wagombea ubunge.Wasifu wa WangweMAREHEMU Chacha Zakayo Wangwe alizaliwa Julai 15, 1956.Nyumbani kwao ni Kijiji cha Kyamakorere, umbali wa kilomita 20 kutoka Tarime Mjini.Alipata elimu ya msingi katika shule za Rosana na Magoto kati ya mwaka 1962 na 1968 kabla ya kujiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya Nyaroha.Baadaye alihamia Dar es Salaam na kujiunga na Sekondari ya Kinondoni Muslim ambako alimaliza kidato cha nne mwaka 1974. Alisoma kidato cha tano na sita katika Sekondari ya Mkwawa kati ya 1975 na 1976.Alijiunga na masomo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1978, lakini hakumaliza.Aliwahi kufanya kazi na Benki ya NBC, Shirika la Kujitolea la Ujerumani, Kampuni ya Lacop na Mgodi wa Dhahabu wa Afrika Mashariki.Kisiasa amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ukiwamo uenyekiti wa tawi la vijana wa Tanu katika sekondari ya Mkwawa, Mwenyekiti wa Wilaya wa Chadema, Tarime, kati ya 1994 na 1998 kabla ya kujiunga na NCCR-Mageuzi ambako alikuwa Mwenyekiti wa Mkoa kati ya 1998 hadi 2000, lakini akarejea tena Chadema mwaka 2002 na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara wa chama hicho.
Full Nondo hii imetoka katika gazeti la HabariLeo

No comments:

Post a Comment