Nafasi Ya Matangazo

April 19, 2024

Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego









Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego amepiga marufuku wananchi wa mkoa huo kuanza kunywa pombe asubuhi badala ya kufanya shughuli za maendeleo na za kiuchumi hali ambayo inaweza kusababisha kudumaa kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi hao na Taifa kwa ujumla.

Mkuu wa mkoa huyo ametoa kauli hiyo katika Kijiji cha Kashangu, Halmashauri ya ITIGI kwenye ziara yake ya kikazi ya Siku Mbili ya kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo ya Elimu na Afya.

HALIMA DENGEGO ameonya kuwa hatasita kuwachukulia hatua Viongozi wa Vijiji na kata ambao watashindwa kudhibiti hali hiyo ya unywaji wa pombe nyakati za asubuhi badala ya kuhimiza wananchi kwenda kufanya shughuli halali za kijitafutia riziki.

“Mnaanza kunywa Pombe asubuhi hasa watoto wa kike hii Sio sawa lazima tusimamiane nikikuta jambo linaenda ndivyo sivyo nitakamata Mtendaji kwa sababu anasheria kama zangu na kwanini ashindwe kudhibiti vitendo hivyo tutawajibishana vikali,” Amesisitiza Halima Dendego.

Kuhusu utoaji wa chakula mashuleni, Mkuu wa mkoa wa SINGIDA amewaagiza Wakuu wa Shule zote za mkoa wa SINGIDA kwa ushirikiano na Viongozi wa Vijiji na kata kuweka utaratibu wa kutoa chakula kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanajifunza kwa bidii.

Amesema utoaji wa chakula mashuleni utasaidia kwa kiasi kikubwa kupandisha ufauli kwa wanafunzi hivyo ni muhimu kwa kila shule kuanza utaratibu wa kutoa chakula kwa wanafunzi wao.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt Fatma Mganga amewataka Watendaji wa Halmashauri na Kata mkoani humo kusimamia vizuri ujenzi wa miradi ya maendeleo hasa umaliziaji wa majengo mbalimbali ili kudhibiti vitendo vya wizi wa vifaa vya ujenzi.

Amesema hatapenda kusikia wala kuona wizi wa vifaa katika miradi ya maendeleo hivyo Viongozi lazima wasimamie kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kuleta manufaa kwa Wananchi na sio vinginevyo.

Katibu Tawala huyo amesema kumekuwa na tabia kuiba vifaa hasa vinapopelekwa kwenye miradi ya maendeleo jambo ambalo linasababisha utekelezaji wa baadhi ya miradi kujengwa chini ya kiwango na kusisitiza kuwa tabia hiyo itakoma iwapo Viongozi wote watashirikiana katika ngazi zote.
Posted by MROKI On Friday, April 19, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo