Nafasi Ya Matangazo

March 17, 2024



Ha
Ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanywa na Serikali  ikiwa ni pamoja na kufanya Marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Mabadiliko hayo yalifanyika Mwaka 2017 yalipelekea kuanzishwa kwa Tume ya Madini na kuvunja Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na TANSORT.
 
Akielezea uanzishwaji wa Tume ya Madini kwa kifupi  Katibu Mtendaji wa Tume, Mhandisi Yahya Samamba  anaeleza kuwa, Tume ya Madini ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kama ilivyorekebishwa mwaka 2017 lengo likiwa ni kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Sera na Sheria ya Madini ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.
 
Akielezea majukumu ya Tume ya Madini kwa ujumla wake, Mhandisi Samamba  anafafanua ni pamoja na kutoa na kusimamia leseni za madini, kusimamia shughuli za utafutaji, uchimbaji, na biashara ya madini, kusimamia ukaguzi wa migodi na mazingira kwa ujumla.
 
Mbali na kupongeza juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mhandisi Samamba  anaeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini wananchi wengi wameshuhudia mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Madini na kuongeza imani kwa Rais na Serikali kwa ujumla.
 
Akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli kabla na baada ya kuanzishwa kwa Tume,  Mhandisi Samamba anaeleza kuwa ukusanyaji wa maduhuli umeongezeka kutoka shilingi bilioni 213.3 katika kipindi cha mwaka wa fedha  2016/17 hadi shilingi bilioni 677.7 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023.

“Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 kama Tume ya Madini tulipewa lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni  822 na kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 677.7  ikiwa ni (82.45%) na katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 tumepewa lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 882 ambalo ninaamini kabisa tutalivuka,” anasisitiza Mhandisi Samamba.
 
Mhandisi Samamba anasema siri ya mafaniko kwenye ukusanyaji wa maduhuli ni pamoja na uzalendo na ubunifu wa  watumishi wa Tume ya Madini Makao Makuu, Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, Maafisa Migodi Wakazi na ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa Wizara ya Madini.
 
Katika hatua nyingine akielezea masoko ya madini yaliyoanzishwa nchini, Mhandisi Samamba anasema kuwa masoko yalianzishwa kama njia mojawapo ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata soko la uhakika la madini yao baada ya kuchimba, Serikali kupata mapato na takwimu sahihi za madini yanayozalishwa na wachimbaji wadogo wa madini, kuuza madini kulingana na bei elekezi inayotolewa na Tume ya Madini kulingana na soko la dunia. Vilevile kudhibiti utoroshaji wa madini kwa wachimbaji na wafanyabiashara wasio waaminifu.
 
Anaendelea kusema kuwa mpaka sasa Tume ya Madini ina masoko ya madini 42 na vituo vya ununuzi wa madini 99 nchini ambayo yameongeza mchango wa wachimbaji wadogo wa madini kwenye mapato kutoka asilimia tano (5) hadi asilimia arobaini (40) Mwaka 2022/2023. 
 
Anasisitiza kuwa masoko ya madini yamepunguza kwa kiasi kikubwa kasi ya utoroshaji wa madini pamoja na kuleta ushindani kwa wafanyabiashara wa madini kupitia masoko na vituo vya ununuzi wa madini.
 
Akielezea mikakati ya Serikali katika udhibiti wa utoroshaji wa madini na kuhakikisha thamani ya madini ya tanzanite inazidi kuimarika, Mhandisi Samamba anasema kuwa mnamo mwaka 2018 Serikali iliamua kujenga ukuta wa Mirerani uliopo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa wachimbaji wa madini hayo na Serikali kwa ujumla.
  
Anaeleza kuwa mikakati mingine iliyowekwa na Serikali ni pamoja na kuwahamisha wafanyabiashara wa madini kutoka jijini Arusha hadi Mirerani lengo likiwa ni kuinua uchumi wa eneo la Mirerani na kudhibiti utoroshaji wa madini.
 
Aidha, anasimulia kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini inaandaa mfumo maalum wa kudhibiti mnyororo mzima wa madini ya tanzanite kuanzia kwenye uchimbaji, biashara, uongezaji thamani hadi usafirishaji wake lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa thamani ya madini hayo inazidi kupaa duniani.
 
Katika hatua nyingine akielezea namna serikali inavyosimamia suala la ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini anasema kuwa kwa kutambua umuhimu wake, mwaka 2018 serikali iliweka kanuni na miongozo mbalimbali ya kuhakikisha watanzania wanashiriki katika shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini kupitia utoaji wa huduma mbalimbali kwenye migodi ya madini kama vile usafiri, bidhaa za kilimo, ulinzi, bima, sheria, benki, n.k.
 
Anasema mpaka kufikia mwaka 2022 asilimia 86 ya bidhaa na huduma zinatolewa na kampuni za kitanzania kwenye kampuni kubwa za uchimbaji wa madini huku asilimia 14 zikitolewa na kampuni za nje ya nchi kupitia kibali maalum kinachotolewa na Tume ya Madini na kwa upande wa ajira katika migodi ya madini asilimia 96 ni watanzania huku raia wa kigeni wakiwa ni asilimia (4) nne

 
“Ieleweke kuwa hakuna kampuni yoyote inayoruhusiwa kuagiza bidhaa au huduma kutoka nje ya nchi bila kupata kibali kutoka Tume ya Madini, lengo letu ni kuhakikisha kila mtanzania ananufaika na Sekta ya Madini,” anasisitiza Mhandisi Samamba.
 
Katika hatua nyingine Tume ya Madini imekuwa ikisimamia kwa makini katika kuhakikisha kampuni za  uchimbaji wa madini zinatoa huduma kwa jamii (CSR) inayozunguka machimbo yake kama Sheria ya Madini inavyoelekeza.
 
Mhandisi Samamba anadokeza kuwa katika mafanikio kwenye Sekta ya Madini suala la usalama kwenye  migodi haliwezi kuachwa nyuma, na katika kutambua hilo Tume ya Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira imekuwa ikifanya kaguzi za mara kwa mara kwenye migodi ya madini pamoja na kutoa elimu.
 
Anaendelea kutaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na  ongezeko la utoaji wa leseni za madini kutoka leseni 5094 katika mwaka wa fedha 2018/2019 hadi leseni 9642 katika mwaka wa fedha 2022/2023. 

Anaongeza kuwa mchango wa Sekta ya Madini kweye Pato la Taifa uliongezeka kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017 hadi asilimia 9.1 mwaka 2022.

Mhandisi Samamba anahitimisha kwa kusema kuwa kampuni nyingi za kigeni zimeendelea kuonesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya Madini kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutangaza fursa zilizopo nchini.
Posted by MROKI On Sunday, March 17, 2024 1 comment

1 comment:

  1. HAKIKA TUME YA MADINI IMELETA MAGEUZI MAKUBWA SANA. HONERENI SANA TENA SANA

    VIONGOZI WETU KWA UBUNIFU WA KULETA MAGEUZI KTK HII SEKTA YA MADINI.

    ReplyDelete

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo