Nafasi Ya Matangazo

July 02, 2022

 
Rais wa Skauti Tanzania na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof. Adolf  Mkenda (Mb) akipokea tuzo ya shukrani kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae ni mlezi wa Skauti Tanzania
Rais wa Skauti Tanzania na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb) akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Skauti Tanzania uliofanyika Jijini Dodoma.
Rais wa Skauti Tanzania na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof. Adolf  Mkenda (Mb) akivalishwa skafu na vijana wa Skauti wakati wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Skauti Tanzania uliofanyika Jijini Dodoma.
Skauti Mkuu Mwantumu Mahiza akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Chama cha Skauti jijii Dodoma
Baadhi ya Skauti Tanzania wakifuatilia hotuba ya Rais wa Skauti Tanzania Mhe.Prof. Adolf Mkenda  (hayupo pichani) wakati wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Skauti Tanzania jijini Dodoma.
************
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof.  Adolf Mkenda (Mb) ametoa rai kwa viongozi wapya wa Skauti Tanzania kuimarisha Skauti shuleni na vyuoni ili kuondokana na changamoto ya  malezi na ukatili wa kijinsia.

Waziri Mkenda ametoa rai hiyo jijini Dodoma alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Chama cha Skauti Tanzania.

Amesema  tabia nyingine zisizofaa ambazo watoto wanakuwa nazo zinasababishwa na kukosekana shughuli tofauti na za darasani ikiwemo michezo na mazoezi ya skauti. 

"Tunahitaji kuimarisha malezi ya watoto wetu ili kuepuka utovu wa nidhamu utakaoweza kusababisha ukatili na unyanyasaji wa kijinsia shuleni," amesema Prof. Mkenda.

Akizungumzia kuhusiana na uchaguzi wa Skauti, Prof. Mkenda amewataka Skauti kuondoa migogoro na kuchagua viongozi waadilifu  watakaoiongoza Skauti vizuri.

Amesema uchaguzi unaofanyika ambao ni wa wajumbe wa Bodi ya Skauti na majina matatu yatakayowasilishwa kwa Mhe Rais kuteua Skauti Mkuu ufungue ukurasa mpya wa utendaji na kwamba kazi kubwa iliyofanywa na viongozi waliotangulia isichafuliwe.

"Niwatake mkaoneshe uadilifu na nidhamu katika utendaji wenu mkiondoa kabisa migogoro iliyopo na kuhakikisha mnalinda jina la chama chetu hiki," amesisitiza Prof. Mkenda.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa  Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wa Zanzibar, Naibu Waziri Ali Abdulgulam Hussein alisema Skauti Zanzibar iko salama na inazidi kuimarika na kwamba kwa mwaka 2021/22 wamefanikiwa kuongeza wanachama na kudumisha umoja. 

Alisema Zanzibar tayari imeshateua majina ya wajumbe ambao wataunda timu ya kusimamia mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Chama Cha Skauti ambayo yanafanyika ili kuzingatia maslahi ya Zanzibar na nafasi ya Zanzibar kwa Tanzania.

Naye Skauti Mkuu, Mwantumu Mahiza amesema Skauti Tanzania imeweka mikakati ya kuondoa utegemezi na kwamba tayari wamepata eneo Jijini Dodoma ambalo litajengwa kambi ya Kimataifa ya Skauti, shule ya michezo, Chuo cha ufundi na kitega uchumi.

Naye Askofu Gervas Nyaisonga ambae ni mmoja wa wadhamini wa Skauti amesema wadhamini wa Skauti wamefarijika kuona Chama cha Skauti kinazidi kuwa na heshima huku kikistawi mikononi mwa viongozi waadilifu.
Posted by MROKI On Saturday, July 02, 2022 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo