Nafasi Ya Matangazo

March 13, 2018




Baada ya kimya cha muda, Africa Magic ikishirikiana na MultiChoice, hatimaye wametangaza rasmi kuanza kwa kinyang’anyiro cha moja ya tuzo maarufu duniani katika tasnia ya sanaa ya filamu zijulikanazo kama Africa Magic Viewers’ Choice Awards (AMVCAs).

Tuzo hizo ambazo hufanyika kila mwaka zimekuwa zikihusisha mamia ya washiriki kutoka kila kona ya bara la Afrika na zimekuwa moja ya tuzo zilizojizolea umaarufu mkubwa barani Afrika na duniani kwa ujumla na limekuwa ni jukwaa muhimu la kutambua na kuenzi vipaji vya tasnia ya filamu katika bara la Afrika.

AMVCAs zilibuniwa kuthamini na kutambua mchango wa watengeneza filamu wa Kiafrika, waigizaji na wataalam katika mafanikio ya sekta ya filamu na televisheni ya bara hili na kutokana na mafanikio ya tuzo tano zilizopita, maandalizi ya tuzo za mwaka huu ambazo zinatarajiwa kuwa kubwa na za kuvutia zaidi yameanza na muamko tayari umeshaanza kuonekana na ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa sana.

Mkurugenzi wa MultiChoice Tanzania Maharage Chande amebainisha kuwa wasanii wa Tanzania sasa wanaweza kuanza kuwasilisha kazi zao kwa ajili ya tuzo hizo na kazi hizo zitaendelea kupokelewa hadi tarehe 30 Aprili 2018.

“Baada ya mapumziko mafupi, tunayo furaha kutangaza kwamba  mwaka 2018 utakuwa na toleo la mwaka wa sita mfululizo wa MultiChoice na Africa Magic kuandaa AMVCAs kwa mafanikio na tunaendelea kujivunia mabadiliko yanayoonekana kwenye nyanja ya filamu tangu Tuzo zilipoanzishwa. Uwekezaji wetu endelevu unaonesha dhamira yetu katika kusaidia kuibua na kuthamini vipaji barani Afrika na tunaamini kwamba toleo la 2018 la AMVCAs litaacha alama kubwa zaidi katika sekta ya utayarishaji filamu ya Afrika kuliko matoleo matano yaliyopita” alisema Maharage.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukishiriki katika tuzo hizi na wasanii wetu wa filamu wamekuwa wakifanya vizuri, lakini mwaka huu tunataka tufanye vizuri zaidi na tuwe washindi katika Makundi mbalimbali ya tuzo hizo kwani uwezo tunao” alisema Maharage na kusisitiza kuwa siri kubwa ni kuhakikisha watanzania kwanza wanawasilisha kazi zao kwa wingi wakati huu na kisha wakati wa kupiga kura ukifika tuhakikishe tunapigia kura kazi zetu na wasanii wetu.

Katika Msimu uliopita, Filamu za Kitanzania ziliwika katika kundi la Filamu Bora kabisa Afrika Mashariki ambapo “Aisha” ya  Amil Shivji, “Naomba Niseme” ya Staford  Kihore, na “Homecoming” ya Seko Shamte zilichaguliwa huku  “Siri ya Mtungi” ikijitokeza kwenye kundi la Filamu Bora za lugha ya Kiswahili

Tanzania ina rikodi nzuri kwenye tuzo hizi kwani misimu iliyopita filamu ya Kitendawili ya Richard Mtambalike ilinyakua tuzo ya filamu bora ya lugha ya Kiswahili wakati Elizabeth Michael ‘Lulu’ alivuma katika tuzo hizo katika filamu yake ya Mapenzi iliyoteuliwa kuwa filamu bora kabisa Afrika Mashariki.

Tuzo hizi za AMVCAs zinahusisha watengeneza filamu katika vipengele mbalimbali kuanzia uigizaji na uongozaji mpaka uandishi na utengenezaji na mwaka huu, tuzo kadhaa katika vipengele mbalimbali zitatolewa kuanzia kwenye uigizaji na uongozaji mpaka uandishi na utengenezaji. Vipengele vingine vitahusisha: filamu fupi au video za kwenye mtandao, muziki, ubunifu wa mavazi, sauti na mwanga kati ya vingi vingine. Kwa 2018 kuna vipengele 27 kwa ujumla, ambapo 7 viko wazi kwa ajili ya kura za watazamaji na 20 vitaamuliwa na jopo la majaji wenye uzoefu mkubwa katika tasnia ya filamu ulimwenguni.

Kuingia AMVCAs ni bure na tarehe ya kufungwa kwa maingizo ni 30 Aprili 2018. Filamu au sinema zilizotayarishwa kwa ajili ya televisheni au tamthiliya za kwenye televisheni ambazo ziliingizwa mwanzoni au kuteuliwa kwa ajili ya tuzo, au kutuzwa zawadi katika shindano lingine la filamu na televisheni zinaruhusiwa kuingizwa kwenye AMVCAs kama zinarushwa au kuoneshwa katika kipindi cha kuanzia Oktoba, 2016 hadi Machi, 2018.

Maelekezo ya kushiriki:

HATUA YA 1
Prepare a 2 to 3 minute long showreel for your online submission. /Andaa ufupisho wa filamu yako wenye muda wakati ya dakika 2 hadi 3 kwa ajili ya kuuwasilisha kwa njia ya mtandao

HATUA YA 2
Ingia www.africamagic.tv na uende kwenye ukurasa wa kuwasilisha.

HATUA YA 3
Jaza fomu za uwasilishaji na upandishe video yako. Namba ya kipekee ya utambulisho itatolewa kwa kila ingizo la mtandaoni lililokamilika. Kisha kutegemea na eneo ulipo, tuma ingizo lake akionesha namba zake za utambulisho.

Kwa maelezo zaidi juu ya mahitaji ya kujiunga na taratibu za uwasilishaji, tafadhali ingia www.dstv.com


Posted by MROKI On Tuesday, March 13, 2018 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo