Nafasi Ya Matangazo

December 06, 2017

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amezitaka taasisi za Serikali kulipa madeni ya ankara za maji kwa mamlaka za maji nchi nzima, ili ziweze kutoa huduma bora ya maji inayokidhi mahitaji ya wananchi. 

Aweso alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Moshi (MUWSA), alipotembelea mamlaka hiyo kwa dhumuni la kujionea utendaji wa mamlaka hiyo mkoani Kilimanjaro. 

‘‘Mamlaka za Maji nchini zimeendelea kukabiliwa na changamoto ya malimbikizi makubwa ya madeni ya ankara za matumizi ya maji kwa taasisi za Serikali, ambazo zimekuwa zikipata huduma ya maji na kushindwa kulipa kwa wakati, ambapo hadi kufikia Machi 2017 deni lilikuwa limefika Sh. bilioni 39.94’’, alisema Naibu Waziri. 

‘‘Kuna haja taasisi za Serikali kulipa madeni yao yote kwa kuwa wamekuwa kikwazo katika maendeleo ya Sekta ya Maji, kwani mamlaka nyingi zimekuwa zikikosa fedha za kutosha kwa ajili ya kujiendesha na kupeleka maji kwa wananchi. Wakilipa madeni hayo itaziwezesha mamlaka zetu kujiendesha kwa ufanisi na kufikia lengo la kuwapa wanachi huduma bora ya maji iliyo endelevu,’’ alisema Aweso. 

Aweso alisema wizara itaangalia jinsi ya kufanikisha ulipwaji wa madeni hayo, ili kuimarisha huduma ya maji mijini kufikia asilimia 86 mwezi Juni, 2017 na 95 ifikapo mwaka 2020 kulingana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi. 

Aidha, Naibu Waziri Aweso ametembelea mradi wa maji wa Same-Mwanga ambao unatekelezwa katika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro kwa nia ya kuhakikisha unatekelezwa vya ubora na kukamilika kwa wakati. 

Mradi huo mkubwa unategemea kuhudumia zaidi wa watu 400,000 wa vijiji 38 katika Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe, unatarajiwa kugharimu zaidi ya Dola za kimarekani milioni 300 na kukamilika Mei, 2019. 
Posted by MROKI On Wednesday, December 06, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo