Nafasi Ya Matangazo

November 15, 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitoa maagizo ya kuvunjwa kwa sehemu ya majengo ya TANESCO (pichani nyuma) na la Wizara ya Maji ili kupisha ujenzi wa miundombinu baada ya kukagua maandalizi  ya ujenzi wa daraja la ghorofa tatu la Ubungo (Ubungo Interchange) jijini Dar es salaam akiwa ameongozana na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa a Dar es salaam Mhe. Paul Makonda mara tu baada ya kuwasili kutokea kijijini kwake Chato mkoani Geita leo Jumatano Novemba 15, 2017.
Wananchi wakimshangilia  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati akitoa maagizo baada ya kukagua maandalizi  ya ujenzi wa daraja la ghorofa tatu la Ubungo (Ubungo Interchange) jijini Dar es salaam akiwa ameongozana na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa a Dar es salaam Mhe. Paul Makonda mara tu baada ya kuwasili kutokea kijijini kwake Chato mkoani Geita leo Jumatano Novemba 15, 2017

Taswira za maendeleo ya ujenzi wa daraja la juu (Fly Over) eneo la TAZARA jijini Dar es salaam kama lilivyo leo Jumatano Novemba 15, 2017
 ****************
Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo Novemba 15, 2017, amerejea jijini Dar es salaam akitokea kijijini kwake Chato, mkoani Geita.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dare es salaam, Rais amepokelewa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda na viongozi wengine wa mkoa.

Baada ya kutoka Uwanja wa Ndege, Rais Magufuli akiwa ameongozana na Makamu wa Rais pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam,amekagua Ujenzi wa Daraja la juu Tazara ( Tazara Fly-Over) na Ujenzi wa Daraja la ghorofa tatu la Ubungo ( Ubungo Interchange)

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Ubungo, Rais Magufuli amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS  Mkoa wa Dar es salaam Mhandisi Ndyamukama Julius kuvunja sehemu ya jengo la TANESCO na jengo la Wizara ya Maji yaliyopo katika eneo la hifadhi ya barabara ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya daraja hilo.

''Sheria ya hifadhi ya barabara katika eneo hilo ni mita tisini kila upande kutoka katikati ya barabara hivyo ni lazima sheria hiyo iheshimiwe ili kuharakisha ujenzi wa Daraja la ghorofa tatu katika eneo hilo la Ubungo uanafanyika bila vikwazo kwani sheria ni msumeno haina budi kuzingatiwa hata na Serikali yenyewe'' amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameiagiza TANROADS kutangaza tenda ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita kumi na sita (16) kutoka eneo linapoishia Daraja la ghorofa tatu katika eneo la Ubungo kuelekea Chalinze ili itanuliwe kwa lengo la kurahisha usafiri katika jiji la Dar es salaam.

Rais Magufuli amewataka Makandarasi wanaojenga Daraja la Tazara na Ubungo kuharakisha ujenzi wa madaraja hayo usiku na mchana ili yaweze kumalizika kwa wakati ama kabla ya muda huo katika kurahisisha maendeleo ya kibiashara katika jiji la Dar es salaam.

''Dar es salaam ni jiji la kibiashara hivyo hakuna budi miundombinu yake ya usafiri iweze kurahisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kutoka ndani ya jiji na nje ya jiji la Dar es salaam'' amesema Rais Magufuli.   

Mhandisi wa Masuala ya Usalama wa Ujenzi Mhandisi Richard Baruani amemueleza Rais Magufuli kuwa Ujenzi wa Daraja la Tazara umefikia asilimia 64 ambapo Daraja hilo linatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2018.

Kwa upande wa Daraja la ghorofa tatu la Ubungo, Mhandisi Mshauri Reginald Kayanga amesema  ujenzi wake unatarajiwa kuanza rasmi Desemba 2017.
Posted by MROKI On Wednesday, November 15, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo