Nafasi Ya Matangazo

May 30, 2016

Dakitari wa macho akiwa katika jukumu la kumpima macho mwanafunzi wa shule ya msingi msasani

Rais wa klabu ya Rotary ya Oyster bay jijini Dar es Salaam, Bwana Mohammed Versi akizungumza na wanahabari

Baadhi ya madakitari wakiwa katika majukumu yao ya kuhakikisha kila mwanafunzi anapata matibabu

Dar es Salaam, 29 Mei 2016
Klabu ya Rotary ya Oyster Bay ya jijini Dar es Salaam imeandaa kambi ya matibabu na kutoa huduma za afya kwa wanafunzi wa shule mbili za Msasani, Msasani A na Msasani B na kufanikiwa kutoa huduma kwa wanafunzi zaidi ya 950. Kambi hiyo ya siku moja ilitoa vipimo vya afya, ushauri, matibabu na huduma mbalimbali za meno, macho, malaria, usafi wa mwili, minyoo, masikio, pua na koo (ENT), pamoja na magonjwa ya ngozi. Kampeni ya Damu Salama pia ilifanyika wakati wa kambi hiyo ili kuwawezesha uchangiaji wa damu katika benki ya damu salama.

Akizungumza na waandishi wa habari, Rais wa klabu ya Rotary ya Oyster bay jijini Dar es Salaam, Bwana Mohamed Versi alisema waliguswa kufadhili upimaji huo kwa sababu suala la afya ni jambo la msingi kwa mwanadamu
"Rotary tumekuwa na utaratibu wa kusaidia jamii, na hii si mara ya kwanza kusaidia shule hii, tayari tumeshajenga maktaba mbili, tumeweka maji safi na salama, tumepanda miti, tumejenga ukuta ili kuimarisha ulinzi na awamu hii tumeona ni vyema tutoe huduma ya afya"

Uongozi wa shule ya msingi Msasani umesema umefurahishwa na kitendo cha klabu ya Rotary ya Oyster Bay kwa kutambua kuwa afya njema ni silaha bora kwa mtoto katika mafaniko ya kielimu.
"Nawashukuru mno Rotary maana wamekuwa washirika waaminifu wa vitendo na si maneno pekee.

Bado tunaomba wadau wengine waige mfano huu katika kutusaidia, bado tuna changamoto mbalimbali zinazotukabili" alisema mwalimu mkuu wa shule hiyo, Egidius Mjumangoma
Kambi hiyo ya matibabu ni muendelezo wa huduma mbalimbali za kijamii zinazotolewa na klabu hiyo katika shule za Msasani A na B. Miradi katika shule hiyo ilianza katika eneo la maji na usafi ambapo shule hizo zilipatiwa maji safi na salama ya kunywa pamoja na ya matumizi mengine.

Klabu hiyo pia ilifanya ukarabati wa majengo na kuweka vitabu katika maktaba mbili kwenye shule hizo. Maktaba hizo zina vitabu vipya na vinavyovutia kwa matumizi ya watoto, makabati yenye vitabu vipya vipatavyo elfu nne (4,000) vingi vikiwa katika lugha ya Kiswahili, ili kutoa hamasa ya kusoma kwa watoto wadogo.

Klabu hiyo ya Rotary Oyster Bay, kwa sasa iko katika ujenzi wa ukuta kuzunguka shule hizo ili kuweka usalama wa mali za shule pamoja na wanafunzi. Ujenzi huo umewezeshwa na fedha zilizopatikana kutoka kwenye mojawapo ya shughuli za ukusanyaji fedha zinazofanywa na klabu hiyo. Mojawapo ya kazi zilizofanyika wakati wa kambi ya matibabu ilikuwa ni ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa ukuta huo ambapo wanaklabu na wageni waalikwa walishiriki katika ziara hiyo.

Kambi hiyo ya matibabu imefanyika kwa udhamini wa Diamond Trust Bank, Whitedent, Knight Support, Vital Supplies, Mansoor Daya, Cello na Sayona kwa ushirikiano na Hindu Mandal Hospital, TDA, Damu Salama na wanafunzi kutoka Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS) na Hubert Kairuki Memorial University (HKMU).

Maktaba hizi mbili zilifadhiliwa chini ya mpango uitwao “Rotary Global Grant”, ambapo katika tafsiri za Rotary, ni pale ambapo Rotary International na ofisi ya Rotary katika kanda husika hutoa msaada wa kifedha kwa klabu yoyote ya Rotary ndani ya kanda. Klabu inayopewa ufadhili huo inatakiwa kushirikiana na klabu yoyote kutoka kanda nyingine ili kuendesha mradi wa jamii ulio endelevu na ambao matokeo yake yanaweza kupimika.

Baada ya shule hizo kuchukuliwa chini ya uangalizi wa Klabu ya Rotary ya Oyster Bay, miradi mingine inapangwa kufanyika katika shule hizo mbili ambapo mafunzo kwa walimu yameandaliwa kufanyika ndani ya mwaka huu. Walimu wa shule hizo watapewa mafunzo ya namna ya kufundisha watoto, yani namna na kutumia maktaba hizo mpya kwa lengo la kukuza kiwango cha uelewa kwa watoto wadogo kwenye jamii zetu.
Posted by MROKI On Monday, May 30, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo